Mwili wa Alexei Navalny kuzuiliwa kwa wiki mbili zaidi ili ufanyiwe 'uchunguzi wa kemikali'
Familia ya Alexei Navalny, mkosoaji wa Putin aliyefariki katika gereza la Urusi, imeripotiwa kuambiwa mwili wake hautaachiliwa kwa wiki mbili.
Mama yake aliarifiwa kuwa mwili wake bado unazuiliwa kwa "uchambuzi wa kemikali", mwakilishi wa Navalny alisema.
Hakujakuwa na uthibitisho wa mahali mwili huo upo kutoka kwa mamlaka ya Urusi, huku juhudi za kuupata zikizimwa mara kwa mara.
Mke wa marehemu kiongozi hyo wa upinzani nchini Urusi ameishtumu mamlaka kwa kuuficha.
Katika video siku ya Jumatatu akiapa kuendelea na kazi yake ya kupigania "Urusi huru", Yulia Navalnaya alimshutumu moja kwa moja Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa kumuua mumewe. Pia alidai mwili wake ulikuwa umehifadhiwa hadi athari za sumu kutoka kwa wakala wa neva Novichok zitakapoisha.
Sauti yake wakati fulani ikitetemeka kwa huzuni na hasira, Bi Navalnaya aliuliza watazamaji kusimama kando yake na "kushiriki ghadhabu na chuki kwa wale ambao walithubutu kuua maisha yetu ya baadaye".
Kifo cha Navalny gerezani kilitangazwa Ijumaa. Wakuu wa gereza la Siberia alikozuiliwa walisema hakuwahi kupata fahamu baada ya kuzirai kufuatia matembezi.
Mama yake na wakili walisafiri hadi gereza hilo lililo mbali mara tu baada ya habari za kifo chake kutokea.
Juhudi za kuupata mwili huo zimekuwa zikizimwa mara kwa mara na chumba cha kuhifadhia maiti cha magereza na viongozi wa eneo hilo.
Siku ya Jumatatu, Kremlin ilisema uchunguzi kuhusu kifo cha Navalny unaendelea na kwamba "hakuna matokeo" hadi sasa.

Post a Comment