MOROGORO KUUNGANISHWA NA MIKOA YA KUSINI KWA LAMI
Serikali kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) imesema imeanza utaratibu wa kujenga Barabara kwa kiwango cha lami kutoka Nachingwea – Liwale – Ilonga – Mwaya hadi Mahenge ambapo ilitangaza zabuni (Expression of Interest) ya kumpata Mhandisi Mshauri wa kufanya kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa Barabara hiyo.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya Bungeni jijini Dodoma Februari 15,2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Ulanga, Mhe. Salim Hasham aliyeuliza Je, kuna mpango gani kujenga barabara ya kiwango cha lami kutoka Liwale hadi Mahenge kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Mikoa ya Kusini.
Eng. Kasekenya amesema Taratibu za manunuzi zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2024 na kusisitiza kuwa baada ya kukamilika kwa kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina na kwa kuzingatia matokeo ya taarifa ya athari za mazingira kwani sehemu kubwa inapita ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Selous, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo.
Aidha, akijibu swali la Mbunge wa Mpwapwa, Mhe. George Malima aliyeuliza Je, nini tamko la Serikali juu ya ujenzi wa Daraja la Godegode – Mpwapwa. Eng. Kasekenya amesema Serikali ilitangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Godegode (Mpwapwa) tarehe 08 Juni, 2022 na zilifunguliwa tarehe 03 Agosti, 2022 lakini hakupatikana mzabuni aliyekidhi vigezo, hali iliyolazimu zabuni kutangazwa upya tarehe 23 Mei, 2023 na kufunguliwa tarehe 18 Julai, 2023 kwa mara ya pili.
Amesema Taratibu za manunuzi zinatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2024 na Mkataba wa ujenzi unatarajiwa kusainiwa mwishoni mwa mwezi Juni, 2024.

Post a Comment