Matapeli waibuka kivingine Facebook, waitumia Unicef
BAADA
ya watu wengi kubaini mbinu za wizi zinazofanywa na matapeli kupitia mitandao
mbalimbali ya kijamii, sasa wamegundua mbinu mpya kwa kulitumia shirika la
kimataifa la kuhudumia watoto (Unicef).
Matapeli
hao, wametengeneza jina linalosomeka kama Unicef African Foundation,
wakijifanya kutoa fedha kwa watu wenye uhitaji, wajasiriamali na wenye maisha
magumu. Fedha zinazotolewa ni shilingi 2,440,000.
Blog
hii ilifanya mawasiliano na watu hao, Unicef African Foundation ambao ili kutoa
fedha hizo, waliuliza maswali kadhaa, yakiwemo sehemu ulikosikia kuhusu habari
zao. Kisha wakataka kujua majina kamili, namba ya simu pamoja na sehemu mtu
huyo alipo.
Baada
ya hapo, matapeli hao walitutumia ujumbe ufuatao :
Hongera,
unastahili kupokea Tsh.2,464,000.00.
Fedha hizi ni kutoka kwa
Wakfu wa UNICEF kusaidia watu wetu ambao lazima wawe katika mazingira magumu.
Mipango yetu inafadhiliwa na wafadhili binafsi, wakfu, biashara na taasisi.
tunatumai unafahamu kuwa ingekugharimu ada ya kuwezesha ya TSH. 61,000.00 ili
maelezo yako yaandikwe kwenye mfumo wetu. Hii ni malipo ya mapema kila wakati.
Tujulishe ukiwa tayari ili tuendelee.
Blog
hii ilifanya mawasiliano na mmoja wa marafiki zake aliyekiri kupokea fedha
kutoka kwa watu hao katika akaunti yake ya Facebook, lakini alipoulizwa ukweli
wa habari hizo, alikataa katakata na kudaki kuwa watu hao walidukua akaunti
yake na hadi wakati huo, alikuwa haipati.
Akasema
kuwa amekuwa akipigiwa simu nyingi na watu wanaomfahamu, wakitaka kujua habari
hizo, ingawa wengine humpigia baada ya kugundua kuwa wametapeliwa.
Blog
hii pia iliingia katika website ya Unicef ambako hakukuwepo na kitu kinachoitwa
Unicef African Foundation Limited na hata ilipojaribu kuwasiliana na Unicef
Tanzania, haikujibiwa.
Blog
hii inaviomba vyombo vinavyohusika kuwatafuta matapeli hao wanaotumia namba ya
simu ya airtel iliyosajiliwa Kenya, 254782529454.
Pia
inawaomba wananchi wote kutosadiki aina yoyote ya mikopo inayowataka
kutanguliza kutoa fedha. Hawa Unicef African Foundation ni matapeli kama
matapeli wengine. WAEPUKE!

Post a Comment