Marekani yaonya mji wa Ukraine unaweza kutwaliwa na Urusi
Marekani imeonya kwamba Urusi inaweza kuuteka mji muhimu wa mashariki mwa Ukraine wa Avdiivka - eneo la mapigano makali zaidi katika miezi ya hivi karibuni.
"Avdiivka iko katika hatari ya kuangukia katika udhibiti wa Urusi," msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa John Kirby alisema, akitoa mfano wa uhaba wa risasi wa Ukraine.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliapa kufanya kila kitu "kuokoa maisha ya watu wengi wa Ukraine iwezekanavyo".
Wanajeshi wa Urusi wamepata mafanikio huko Avdiivka, na kutishia kuuzingira.
Mji huo - ambao umekaribia kuharibiwa kabisa - unaonekana kama lango la kuingilia karibu na Donetsk, mji mkuu wa eneo la Ukraine uliotekwa na wapiganaji wanaoungwa mkono na Urusi mwaka 2014 na baadaye kunyakuliwa kinyume cha sheria na Moscow.
Rais wa Urusi Vladimir Putin alianzisha uvamizi kamili wa Ukraine mnamo tarehe 24 Februari 2022.
Katika mkutano wa Alhamisi mjini Washington, Bw Kirby alisema Avdiivka inaweza kuanguka kwa kiasi kikubwa "kwa sababu vikosi vya Ukraine vilivyoko ardhini vinaishiwa na risasi za kivita".
"Urusi inatuma wimbi baada ya wimbi la vikosi vya askari kushambulia maeneo yanayoshikiliwa na wanajeshi waUkraine," alisema.
"Na kwa sababu bunge la Congress bado haijapitisha muswada wa nyongeza ya msaada, hatujaweza kuipatia Ukraine mizinga ambayo wanahitaji sana kuvuruga mashambulio haya ya Urusi.
BBC

Post a Comment