Marekani yaionya Iran dhidi ya kuisambazia Urusi silaha

 


Serikali ya Marekani imeionya Iran kwamba ikiwa itapeleka makombora ya balistiki kwa Urusi, itakabiliwa na majibu ya "haraka na makali" kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

Haya yanajiri baada ya shirika la habari la Reuters kuripoti mapema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilituma aina hizo za silaha nchini Urusi.

John Kirby, msemaji wa Baraza la Usalama la Ikulu ya White House, aliwaambia waandishi wa habari siku ya Alhamisi kwamba Marekani bado haijaona ushahidi wa kuthibitisha kuhamishwa kwa makombora hayo kutoka Iran hadi Russia.

Shirika la habari la Reuters liliripoti siku ya Jumatano, likinukuu vyanzo sita, kwamba Iran ilituma idadi kubwa ya makombora yenye nguvu ya balestiki hadi Urusi.

Bwana Kirby alisema: "Ripoti inasema kwamba Wairani wanaonyesha wazi kwamba watatuma makombora ya balestiki nchini Urusi. Hatuna sababu ya kufikiria kwamba hawatachukua hatua juu ya hili."

Ameongeza kuwa: "Sisi kwa upande wetu tunalizungumzia suala hili katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Tutaweka vikwazo vipya dhidi ya Iran na tutazingatia chaguzi zaidi kama jibu kwa uratibu wa washirika wetu barani Ulaya na kwingineko duniani."

Katika ripoti yake, shirika la habari la Reuters, likinukuu vyanzo vitatu vya habari nchini Iran, liliandika kuwa Iran imetuma takribani makombora 400 kwa Urusi, yakiwemo idadi kubwa ya makombora ya masafa mafupi ya Fateh-110, kama vile mfumo wa rununu wa Zulfiqar, unaoweza kuangazia eneo kati ya kilomita 300 na 700.

Shirika la habari la Reuters liliandika kuwa, shehena ya silaha hizo ilianza kusafirishwa mapema Januari, yaani baada ya makubaliano kukamilika mjini Tehran na Moscow mwishoni mwa mwaka jana kati ya jeshi na mamlaka ya nchi hizo mbili.

Bwana Kirby alisema kuwa Iran imeuza nje idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani, mabomu ya kuongozwa na risasi za kivita kwa Urusi, ambazo nchi hiyo ilitumia katika vita vya Ukraine.

Amesema: "Katika kukabiliana na Iran kuendelea kuunga mkono vita vya kikatili vya Russia, tutaweka vikwazo zaidi dhidi ya Iran katika siku zijazo, na tuko tayari kuchukua hatua hiyo.

No comments