Kelvin Kangethe: Mtoro wa Marekani anayesakwa kwa mauaji atoroka kizuizini nchini Kenya

 


Mwanaume mmoja aliyekimbia Marekani baada ya kudaiwa kumuua mpenzi wake ametoroka kutoka kituo cha polisi cha Kenya alikokuwa akishikiliwa bila mtu yeyote kumzuia.

Kelvin Kangethe, 41, alikamatwa wiki iliyopita akitoka katika klabu moja katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, baada ya msako wa miezi kadhaa.

Mahakama ilikuwa imeruhusu kuzuiliwa kwake kwa siku 30 akingojea uwezekano wa kurejeshwa Marekani.

Mamlaka zinasema kuwa baada ya Bw Kangethe kumuua mpenzi wake Oktoba mwaka jana, aliuacha mwili wake kwenye gari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Boston Logan.

Kisha akapanda ndege kuelekea Kenya, nchi yake ya asili.

Hajazungumzia madai hayo.

Polisi wamewashangaza Wakenya kwa kufichua kwamba Bw Kangethe alifanikiwa kutoka katika Kituo cha Polisi cha Muthaiga alikokuwa akizuiliwa Jumatano mchana.

Kulingana na taarifa ya polisi, Bw Kangethe aliondoka wakati wa mkutano katika chumba cha kibinafsi na mwanamume aliyezuru kituo hicho akisema ni wakili wake.

"Baada ya muda mfupi mfungwa alitoroka kwa kukimbia na kumwacha wakili," ilisema taarifa hiyo.

Wakati huo, maafisa wote walikuwa wakihudhuria mkutano tofauti ambao ulikuwa umeitishwa na mkuu wa kituo hicho.

Shahidi mmoja anayefanya kazi karibu na kituo hicho aliambia BBC kwamba polisi walimfuata Bw Kangethe, ambaye alikuwa amevalia koti jeusi.

"Tulidhani alikuwa anafukuzwa kwa ajili ya kuvuka barabara bila kuwa mwangalifu. Watu walimtazama tu akikimbia," shahidi huyo alisema.

"Kama tungejua kwa nini anatafutwa tungesaidia kumkamata."

Polisi wanasema walishindwa kumkamata Bw Kangethe.Kwa sasa hajulikani alipo.

Maafisa wanne wa polisi waliokuwa kazini na mtu aliyekutana na Bw Kangethe wamekamatwa, kamanda wa polisi wa Nairobi Adamson Bungei aliambia vyombo vya habari vya eneo hilo.

Gazeti la kibinafsi la Star lilimnukuu Bw Bungei akisema kuwa kufeli huko kwa maafisa wa usalama ni "aibu" kwa polisi wa Kenya, ambao wameanzisha msako mpya wa kumtafuta Bw Kangethe.

Maafisa katika kituo hicho wanazuia watu kuingia kituoni i, wakihofia habari zaidi zinaweza kuvuja kwa umma.

Familia ya mpenziwe Bw Kangethe, Margaret Mbitu, iliambia vyombo vya habari vya Marekani kwamba alikuwa akipanga kusitisha uhusiano wao kabla ya kudaiwa kumuua.

Alikuwa muuguzi Mkenya Mmarekani mwenye umri wa miaka 30 anayefanya kazi huko Halifax, Massachusetts.

Bi Mbitu alionekana kwa mara ya mwisho akiwa hai akitoka kazini jioni ya tarehe 30 Oktoba mwaka jana.

Aliripotiwa kutoweka siku hiyo hiyo na mwili wake uligunduliwa siku mbili baadaye.

Mamlaka zinaamini kuwa Bw Kangethe aliondoka Marekani kati ya kutoweka kwa Bi Mbitu na kupatikana kwa mwili wake.

Walimhusisha Bw Kangethe na mauaji hayo baada ya kanda za usalama kumnasa akitoka kwenye maegesho ya uwanja wa ndege ambapo mwili wa Bi Mbitu ulipatikana baadaye.

Alipanda ndege asubuhi baada ya Bi Mbitu kutoweka.

Mahakama ya Kenya ilipaswa kutoa uamuzi Ijumaa ikiwa Bw Kangethe ashtakiwe nchini Kenya au arejeshwe nyumbani ili kujibu mashtaka ya mauaji ya daraja la kwanza nchini Marekani, baada ya kudai kuwa aliukana uraia wake wa Marekani mwaka jana.

No comments