Mwanafunzi raia wa China apatikana Marekani baada ya 'kutekwa nyara kwa njia ya mtandao



Mwanafunzi wa masuala ya biashara ya fedha za kigeni wa China amepatikana akiwa ameganda lakini akiwa hai nchini Marekani baada ya wazazi wake kutapeliwa makumi ya maelfu ya dola katika tukio la "utekaji nyara kwa njia ya mtandao".

Kai Zhuang aligunduliwa "akiwa amezidiwa na baridi sana na mwenye hofu" katika hema moja katika kijiji cha Utah, Polisi wa Riverdale walisema katika taarifa.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 17 anaaminika kujitenga baada ya kudanganywa na watekaji nyara.

Wazazi wake walidanganywa kulipa karibu $80,000 (£62,600).

Zhuang ni mmoja wa wanafunzi wa kigeni wanaolengwa na wale wanaoitwa watekaji nyara wa mtandaoni nchini Marekani hivi karibuni, Polisi wa Riverdale waliongeza katika taarifa yao.

Polisi wanaamini kuwa Kai alikuwa akidhibitiwa na watekaji nyara mapema Desemba 20, alipoonekana na maafisa wa Provo, Utah, akiwa amebeba vifaa vya kupigia kambi.

Maafisa hao walipanga arejeshwe Riverdale, ambako aliishi na familia iliyompokea, kutokana na wasiwasi wa usalama wake. Hata hivyo, hakutaja vitisho vyovyote wakati huo.

Polisi waliwasiliana mnamo tarehe 28 Desemba na shule aliyokuwa akisoma, ambayo ilikuwa imewasiliana na wazazi wake nchini China.

Wazazi wa Kai walikuwa wamewaambia maafisa wa shule kuwa wametumwa ombi la fidia na picha ya mtoto wao ikionesha kuwa alitekwa nyara.

Kulingana na polisi, waathiriwa wa utekaji nyara wa mtandao hushawishiwa kujitenga, na hata kupiga picha zao ili ionekane wanashikiliwa, licha ya watekaji nyara kutokuwepo.

Badala yake, mwathirika anafuatiliwa kupitia Facetime au Skype.

Wote mwathiriwa na familia zao basi wanashawishika kuwa mwingine atadhurika ikiwa hawatatii.

Lakini licha ya watekaji nyara hao kutokuwa na Kai, polisi huko Utah bado wanahofia usalama wake, wakieleza halijoto ya mwezi Disemba ilimaanisha kuwa kuna hatari ya "kuganda hadi kufa usiku kucha".

No comments