Kwa Dkt Nchimbi, upele umepata mkunaji


Mwandishi Maarufu, H. Jackson Brown wa kitabu, “Life's Little Instruction Book,” amepata kusema, “Opportunity dances with those who are already on the dance floor”, kwa tafsiri isiyo rasmi ni kuwa “Fursa hucheza na wale ambao tayari wapo kwenye jukwaa la kucheza”. Ukiangalia kwa sifa, uwezo na uzoefu tayari jina la Dr. Emmanuel Nchimbi lilikuwa likicheza zaidi kwenye nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM kuliko kada mwingine yoyote. Na pengine hili ndilo lililodhihirika baada ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa hapo jana waliporidhia kwa kauli moja pendekezo la kumchagua Dr. Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wa CCM hapo jana. 


CCM imepata?


Jibu la ndio au hapana litategemeana na hoja za mahitaji ya wakati na hali ya kisiasa ndani na nje ya CCM. Dr. Emmanuel Nchimbi anajulikana kama bingwa wa mikakati na mtu wa siasa za masuala. Lakini pia ana sifa ya kuwa na msimamo usio “yumba yumba” huku akibebwa na tabia ya utii na kukubali maridhiano. 


Ni aina ya Mwanasiasa aliyejengwa na kujijenga. Dr. Nchimbi alianzia kuwa Mwenyekiti wa Chipukizi ngazi ya Mkoa, Kabla ya Kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa NEC mwaka 1997. Mwaka 1998 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM(UVCCM) Taifa. Ndiye Mwenyekiti pekee wa UVCCM tangu kuanzishwa kwake kuchaguliwa kwa awamu mbili mfululizo. Kisha akahudumu kama Mkuu wa Wilaya ya Bunda. Mwaka 2005 alimshinda aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Laurence Gama kwenye kura za maoni kisha kushinda Ubunge kwenye jimbo la Songea Mjini. 


Mwaka 2006 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo kisha alihamishiwa Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana(2008) na baadae 2010, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa nafasi hiyo hiyo ya Naibu Waziri. Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, Dr. Nchimbi aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo. Baadae alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani mwaka 2012. Baada ya kujiuzulu mwaka 2013, Dr. Nchimbi aliendelea kuhudumu kama Mbunge wa Songea Mjini hadi 2015 alipotangaza kutokugombea nafasi hiyo. Jambo hili lilileta simanzi kubwa, na maneno yakadai anaenda kugombea Urais. Hata hivyo hakugombea na mwaka 2016 aliteuliwa kuwa balozi wa Tanzania nchini Brazili Mpaka 2021. Kisha aliteuliwa tena Mhe. Rais Dr. Samia kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri mwaka 2022 hadi 2023 alipomaliza muda wake. 

Ndani ya CCM, Dr. Nchimbi amekuwa mjumbe wa wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa miaka 19 na Mjumbe wa Kamati Kuu kwa Miaka 14. Kwa miaka 35 amegubika siasa za CCM na Taifa kama Mtumishi wa Umma(Public servant), Mbunge na Waziri(Member of Parliament and Minister), Kiongozi wa Chama(Party Leader) na Mwanadiplomasia(Diplomat). 


Kwa kuzingatia mahitaji wa wakati na hali ya kisiasa, CCM imepata mtu anaweza kukidhi matarajio ya Wanachama. Uteuzi wake umepokelewa kwa furaha kubwa na Wanasiasa Vijana ndani ya CCM. Wengi wanamuita senior au big brother kutokana na kazi aliyoifanya wakati akihudumu kama Mwenyekiti wa UVCCM Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu. Upinzani wanamuona kama Mwanasiasa wa Masuala na asiyependa Uonevu. Ni aina ya Mtendaji ambaye ataweza kuakisi maridhiano na siasa za hoja. Anajua vema siasa za CCM hazihitaji visasi hivyo atasaidia kwa kiwango kikubwa kuweka makundi ya ndani Pamoja kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadae mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa Mwakani. Utii wa Dr. Nchimbi kwa CCM na Mwenyekiti wake ni jambo lisilo na mashaka. Hotuba yake aliyoitoa wakati ameteuliwa kubwa Balozi wa Tanzania nchini Brazili inaonesha ni mtu anayetii ingawa pia ni mwenye misimamo. Na kwa kiwango kikubwa yupo tayari kuweka pembeni matamanio yake (Kama binadamu mwingine) inapokuja maslahi ya CCM. 


Hivyo, Balozi Dr. Emmanuel Nchimbi amepata nafasi ya Katibu Mkuu, na CCM imepata Katibu Mkuu. Jana Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM Yusufu Makamba amesema, “Upele umepata Mkunaji”, naamini pia, “Mkunaji” amepata Upele, Apewe nafasi ya Kukuna uwo Upele!


Francis Daudi

Kwembe, Dar es salaam

No comments