Kigwangala ana hoja, ila si mtu wa kuaminika
Na Ojuku Abraham
Ni jambo la msingi sana kufuatilia siasa za Chama Cha Mapinduzi (CCM), siyo tu kwa sababu ni chama tawala, bali pia kihistoria. Hakuna namna ambavyo Mtanzania anaweza kuwa kando ya chama hiki, hata kama ni mfuasi wa vyama vingine.
CCM ni chama ambacho kimeshikilia roho za wananchi wote kwa sababu wanachama wake ndiyo wanaokwenda kuunda serikali. Mtu anayesimamia afya za Watanzania ni Waziri anayetokana na chama hiki, kama ambavyo wapo watu wengine katika maeneo muhimu kama elimu, ulinzi, kilimo, mawasiliano, uhusiano wa kimataifa, nishati na kadhalika.
CCM ni chama ambacho ni vigumu raia kutokitaja, hata kama ni kwa ubaya. Hakuna chama mbadala kinachoweza kubeba mizigo ya chama hiki kwa sasa.
Ni kutokana na umuhimu huo, ndiyo maana ili uende sambamba kisiasa katika nchi yetu, chama tawala lazima kiwe kituo cha kwanza cha kuanzia.
Uteuzi wa nafasi mbalimbali za kiserikali unaofanywa na viongozi kwa makada wa chama hiki, hutazamwa kwa jicho pana na Watanzania wote na ndiyo maana maoni mbalimbali hutolewa dhidi ya teuzi hizo, kupitia vijiwe vya kahawa, maofisini, katika mitandao na hata kwenye vyombo vya habari.
Watanzania tunajuana. Tunajua kabisa kwamba huyu, hili analolisema linatoka moyoni, kwa maana anamaanisha, lakini pia tunaelewa pale mtu anaposema neno akiwa kinyume chake.
Aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Afya na baadaye Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Hamis Kigwangala ambaye kwa sasa ameondolewa katika nyadhifa hizo, anafikirisha.
Siku chache zilizopita, akihojiwa na Jenerali Ulimwengu, pamoja na mambo mengine, alidokeza juu ya vigogo wa nchi walivyo na uwezo wa ajabu wa kifedha, kiasi cha mmoja wao kununua jumba lenye thamani ya shilingi bilioni 25 kule Dubai.
Kana kwamba haitoshi, akadai yupo mwingine, amenunua nyumba pale Masaka kwa bei ya dola milioni sita za kimarekani. Dola milioni sita,unaongelea karibu shilingi bilioni 15!
Ukiachana na tuhuma hizo, mbunge huyu wa Nzega, siku chache zilizopita, kupitia akaunti zake kwenye mitandao ya kijamii, alidokeza juu ya kupata vitisho kutoka kwa watu ambao ameamua kutowataja kwa sasa.
Katika kujitetea, Kigwangala anasema pamoja na kwamba yeye hakumtaja mtu kwenye tuhuma alizotoa, lakini haiondoi ukweli kwamba mifumo yetu ya kiuongozi ina kasoro zinazopaswa kurekebishwa.
Ametoa kasoro hizo za kimfumo za uongozi, sheria na nyanja zingine, akisema mambo hayo yanafifisha juhudi za nchi kusonga mbele.
Binafsi ninaunga mkono kwa asilimia nyingi madai ya kijana huyu msomi. Ni kweli kwamba wengi wa viongozi wetu wana makandokando ya kiuadilifu, hasa katika eneo la kujilimbikizia mali.
Hata hivyo, hili linabakia kuwa jambo la hisia tu kwa vile ni vigumu kuthibitisha pasipo shaka. Na hata maoni yake juu ya mifumo ya kiuongozi na kisheria, ina mantiki.
Lakini tatizo langu kubwa, je Kigwangala anaaminika? Hajanyi haya baada ya kuondolewa nje ya mfumo?
Kama nilivyosema pale mwanzo, ni ngumu sana kufuatilia siasa za nchi hii pasipo kwanza kuanza na CCM.
Kigwangala ni mbunge kwa karibu mihula miwili sasa. Kwamba ameenda shule, hili sina tatizo nalo hata kidogo.
Lakini juu ya ubovu wa mifumo ya uongozi anayoizungumzia, ameiona baada ya kuondolewa uwaziri?
Tunayo mifano ya viongozi wengi wanaotokana na CCM kuanza kuzungumza ubaya, ufisadi na hata ubovu wa mifumo au taasisi, wakiwa nje, lakini hubakia kimya wakiingia katika mfumo.
Hii inatufanya tusite kuwaamini kwa sababu kesho wakipewa ulaji, watatuacha solemba. Dkt. Harrison Mwakyembe huko nyuma aliwahi kulalamikia sana jeshi la polisi, lakini alipopewa uwaziri, hakutuonyesha mchango wake katika kumshauri Rais juu ya marekebisho ya jeshi hilo ili liwe bora.
Luhaga Mpina anapiga sana kelele sasa hivi bungeni akiibua kashfa kadhaa za ubadhilifu. Lakini mbona hakusema haya huko nyuma, ila anakuja kusema sasa baada ya kuondolewa uwaziri?
Tungefurahi sana kama tungempata mwana CCM ambaye atatoa kasoro za serikali kabla hajapewa nafasi na akipewa, atuonyeshe kwa vitendo juu ya kile alichokua akipigia kelele, vinginevyo ni vigumu kuwaamini!

Post a Comment