Elimu bado haijatolewa vya kutosha Uhifadhi wa mazingira

 

Na Ojuku Abraham

Kwa miaka mingi, nchi imekua ikiendelea kuathirika taratibu katika sekta ya uhifadhi wa mazingira, kutokana na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu jambo hili, hasa kwa ngazi za chini zaidi ambazo ni familia.

Vyombo vingi vya umma vilivyoundwa kusimamia mazingira, likiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), vimekuwa vikitoa elimu ya uhifadhi wa mazingira katika ngazi kubwa, hasa kwenye semina, makongamano, warsha na kampeni mbalimbali za muda mfupi.

Mikusanyiko hiyo imekua ikiwakutanisha wataalamu, watumishi wa umma, waandishi wa habari, watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Miji na mara chache, watendaji wa serikali ngazi za vijiji, vitongoji na kaya.

Ushahidi wa kimazingira unaonyesha kwamba, kumekuwa na matokeo chanya machache katika maeneo mengi yanayohubiriwa katika semina na makongamano hayo, hasa kwa vile wengi wa washiriki, siyo watu ambao wanaguswa moja kwa moja na wajibu wa kuhifadhi na kutunza mazingira.

Vyombo vingi vya umma, ambavyo kimsingi vilipaswa kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na janga hili, baadhi yao vimeonekana kuwa sehemu ya tatizo kwenye kampeni nyingi za kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

Kwa mfano, wakati kampeni nyingi zimekuwa zikielekezwa katika kuelezea ubaya wa ukataji miti ovyo katika misitu asilia na iliyopandwa, vyombo vya umma vimeendelea kuruhusu magunia kwa magunia ya mikaa yakiingizwa mijini kwa ajili ya matumizi ya kila siku ya shughuli za kibinadamu.

Ingawa hakuna takwimu rasmi, lakini upo uwezekano mkubwa kwamba angalau ekari kadhaa za miti zinakatwa kila siku kwa ajili ya mkaa pekee Tanzania nzima, kitu ambacho hakiendani na kasi ya upandaji miti kote nchini.

Ukiacha miti inayokatwa kwa ajili ya kutengeneza mkaa, lakini pia inakatwa kwenye shughuli zingine za kibinadamu kama ujenzi wa makazi, miundombinu, samadi za maofisini na majumbani, achilia mbali misitu inayopotea kutokana na majanga kama vile moto, mafuriko, vimbunga na kadhalika.

Uharibifu huu wa misitu, hauishii tu katika kumpa athari binadamu kwa maana ya kukausha vyanzo vya maji na kukaribisha jangwa, lakini pia huwakuta hadi wanyama, wanaofungwa na wa porini. Vyanzo vya maji vinapokauka kutokana na shughuli za kibinadamu, husababisha mifugo kukosa sehemu ya kupata maji ya kunywa.

Hali hii ni bora kwa mifugo ifungwayo, ambayo wamiliki wao wanaweza kuwatafutia namna nyingine ya kuwapatia maji, lakini inapotokea kwa wanyama wa porini walio mbugani, huwafanya kuhama kutoka eneo moja kwenda lingine pasipo utashi wao.

Ushahidi usio shaka unaonyesha jambo hili linapofanyika, yapo madhara ambayo yametokea, yakimuathiri binadamu. Wanyama hawa wanaohama kwa kukimbia moto unaowashwa makusudi katika mapori na hifadhi, huwafanya wanyama hao kwenda karibu na makazi ya watu na kufanya uharibifu wa mashamba na wakati mwingine hata kujeruhi na kuua wananchi.

Ukiachana na uharibifu wa misitu ambayo mojawapo ya athari zake ni pamoja na kukauka kwa vyanzo vingi vya maji, lakini hata mazingira ya kawaida ya jamii ya Kitanzania, yako shaghalabaghala. Kumekuwa na uduni mkubwa na ukosefu wa elimu juu ya namna bora ya kukabiliana na changamoto za mazingira tunayoishi, ambayo kwa nyakati tofauti yamesababisha magonjwa ya mlipuko, uharibifu wa miundombinu na athari zisizoepukika.

Ujenzi wa makazi na miundombinu yake limekuwa ni tatizo sugu kwa miaka na miaka sasa. Kwa makusudi au kutojua, baadhi ya watu wamekuwa wakivamia maeneo pasi na kupata baraka kutoka mamlaka zinazohusika, kitu ambacho husababisha hata ramani za kuweka miundombinu kwa ajili yao kuwa migumu.

Badala ya wananchi kwenda katika maeneo yaliyopimwa ambayo ramani zitasomeka vyema ili kurahisisha uwekaji wa miundombinu, wengi hutanguliza makazi kwanza, kitu ambacho huiwia vigumu serikali katika kufanikisha kwa ufasaha ujenzi wa barabara, mitaro ya kukinga maji, usambazaji wa huduma muhimu kama umeme na maji, sehemu za huduma za afya na hata elimu.

Tumeshuhudia mara kadhaa, migogoro ikijitokeza kati ya wanakijiji na baadhi ya hifadhi zilizotengwa, ama wananchi wakidai maeneo hayo ni yao, au wakilazimisha kuingia hifadhini kwa ajili ya kupata mahitaji ya vitoweo kutoka kwa wanyama pori waliomo ndani yake.

Mara kadhaa, jambo hili limesababisha uhasama mkubwa baina ya watumishi wa serikali na wanakijiji wanaolizunguka eneo husika. Kutokana na uhasama huu ambao siyo wa lazima, matokeo yake hifadhi ambazo ni muhimu kwa maisha ya wote, wanyama na binadamu, huhujumiwa makusudi.

Kama nilivyotangulia kusema kule juu, tatizo kubwa linalofanya janga hili la ukosefu wa uhifadhi wa mazingira ulio bora, ni kutokuwepo kwa elimu ya kutosha, hasa kwa kada ya chini zaidi, inayoanzia ngazi ya familia. Pengine kutokana na gharama au muda, lakini elimu kwa familia ndiyo muarobaini wa uhakika katika kukabiliana na suala hili.

Kama baba, mama na watoto watatambua ubaya wa kukata miti ovyo, kutupa taka kiholela na vitu vingine kama hivi vinavyoathiri mazingira, ni wazi kuwa hawa watu watakuwa walinzi wa kwanza wa kuhakikisha jambo hili halifanyiki.

Ninafahamu mbinu mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili kuhakikisha elimu inawafikia walengwa, kama vile vipindi katika redio na televisheni, makala kwenye magazeti na hata kwa kutumia mitandao ya kijamii. Pamoja na hayo, nina wazo ambalo linaweza kusaidia kusambaza elimu zaidi kwa familia.

Watumishi wa umma, wenye utaalam na mambo ya uhifadhi, kama walivyo mabwana na mabibi shamba, kwa kutumia viongozi wa serikali ngazi za vitongoji na vijiji, wawe na vipindi maalum vya kuelimisha umma kwa kuzungumza nao ‘live’.

Zoezi hili linaweza kuanza kwenye maeneo ambayo yapo karibu au kuzunguka sehemu maalum zilizotengwa kama hifadhi, ziwe za misitu, mapori hengefu au hifadhi za wanyama pori. Hapa ni vyema nikaeleweka. Jamii iielimishwe na siyo kulazimisha kuelimisha.

Mtu anapaswa kuelezwa kwamba elimu anayopewa ni kwa faida yake mwenyewe, kwanza kwa ajili ya kulinda mazingira yake ya sasa na baadaye, kumnufaisha yeye na kizazi chake na pia, nini athari zake endapo hiki na hilki kitafanyika, iwe kwa jamii au kwa mtu mmoja mmoja, ikiwa ni pamoja na adhabu ya kisheria kwa wanaokiuka taratibu makusudi.

Elimu hii inapaswa kuanza kwa kuandaa watoa elimu wenyewe. Tunao wataalam wa nyanja mbalimbali katika hifadhi, lakini bahati mbaya si walimu wazuri kwa jamii. Tunahitaji mtu anayeweza kuongea maneno machache ya kueleweka kuliko mtu mwenye Phd, anayeongea misamiati migumu kwa watu ambao huenda hawajaenda shule kwa ngazi kama yake.

 

 

 

 

 

No comments