Ajali ya ndege Japan: Abiria wasimulia misukosuko waliyoipata ndani ya ndege
Ni tukio la kushtusha, ndege ya Airbus A350 iliyobeba abiria 379 ilipogongana na ndege nyingine wakati wa kutua katika uwanja wa ndege wa Tokyo.
Moto na moshi huku ndege ikikimbia kwenye njia ya kurukia.
Muda wa kujiokoa, abiria walikuwa wanatoka kwenye ndege wakikimbia moshi, wakijua kwamba maisha yao yalitegemea sekunde chache zijazo.
Abiria wote waliokuwa kwenye ndege ya Japan Airlines 516 walipona.
Wataalamu wanasema teknolojia mpya ilisaidia kwa sehemu kubwa kuokoa maisha yao ingawa wale waliokuwa kwenye ndege ya pili, ndege ndogo ya walinzi wa pwani - iliyokuwa inapeleka misaada kwa waathiriwa wa tetemeko, hawakupona wote. Watano walifariki na rubani amejeruhiwa vibaya.
Wachunguzi wanatafuta sababu ya kile kilichotokea katika uwanja wa ndege wa Haneda, kujua kwa nini ndege mbili zilikuwa kwenye njia moja ya kurukia kwa wakati mmoja.
Abiria kwa jina la Swede Anton Deibe, 17, alielezea misukosuko aliyopitia baada ya athari ya ajali hiyo ya moto katika ndege.
"Ndege yote ilijaa moshi ndani ya dakika chache," aliliambia gazeti la Uswidi la Aftonbladet.
"Moshi ndani ya ndege uliuma. Kisha milango ya dharura ikafunguliwa na tukajitupa. Hatukujua tunakwenda wapi kwa hivyo tulikimbia tu uwanjani. Hali ilikuwa mbaya sana."
Yeye, wazazi wake na dada yake walifanikiwa kutoka kwenye ndege bila kujeruhiwa.

Post a Comment