Watu 40 wafariki katika maporomoko ya udongo DR Congo

Watu 40 wamethibitishwa kufariki kutokana na maporomoko ya udongo na mafuriko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Jumanne.

Wakazi wamekuwa wakichimba matope kutafuta maiti. Baadhi ya watu wamesombwa na maji ya mafuriko.

Takriban watu 20 walikufa Bukavu, na wengine 20 pia waliuawa katika kijiji cha Burinyi, kilomita 50 kutoka Bukavu.

Mamlaka ya mkoa imesema kuwa inatathmini hali hiyo ili kutoa usaidizi unaohitajika kwa jamii zilizoathirika.

Siku ya Jumanne, tukio sawia na hilo lilitokea Kasai, jimbo la kati, na kusababisha vifo vya watu 20 na kuharibu miundombinu mingi.

Mafuriko na maporomoko ya udongo hutokea mara kwa mara nchini DRC na mara nyingi yanakuwa mabaya zaidi kutokana na msongamano wa watu mijini na miundombinu dhaifu, ambayo imefanya jamii kuwa hatarini zaidi.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, mabadiliko ya hali ya hewa yamesababisha mvua kubwa katika baadhi ya sehemu za bara Afrika, na matokeo yake ni mabaya.

DR Congo ni mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, licha ya rasilimali zake nyingi za madini.

Pia imekumbwa na migogoro ya kivita mara kwa mara.

No comments