Wanaume wanaovaa size 40, wanawake size 35 afya zao zipo hatarini- Profesa Janabi
Amesema kasi ya ongezeko la Wagonjwa wa Figo inaonesha wazi Watu wengi wana mtindo wa Maisha usiofaa ikiwemo ulaji mbaya wa Vyakula, Matumizi makubwa ya Pombe na Dawa za Kutuliza Maumivu bila utaratibu mzuri pia kutofanya mazoezi.
Ameongeza kuwa tafiti zinaonesha 90% ya Watu hawajui kama Figo zao zina matatizo huku 40% wakifika Hospitali wakati Ugonjwa ukiwa hatua ngumu na za mwisho kutibika na hauwezi hata kusafisha Damu (Dialysis).
Kwa mujibu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), ili kuepuka Magonjwa yanayotokana na Vyakula, Watu wanapasawa kutotumia Vyakula Vilivyopikwa kwa Mafuta Mengi, Vinywaji Venye Sukari Nyingi zikiwemo Soda aina zote na Juisi za Viwandani.
Unachokula ndicho huamua afya yako ya figo, ndicho anachomaanisha Profesa Mohamed Janabi akisema sababu ya tatizo la figo ni vyakula anavyokula mtu.
“Kisukari ndio ugonjwa namba moja unaosababisha tatizo la figo, kisukari ni tatizo linalotokana na ulaji na ulaji unarekebishika,” anasema Profesa Janabi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) wakati wa uzinduzi wa taasisi ya Profesa jay inayolenga kutoa misaada kwa wagonjwa wa figo.
Ili kukabiliana na unene wa kupitiliza, kwa siku 30, Profesa Janabi anashauri mtu akiamka asubuhi asinywe chai kama kawaida, bali asogeza muda hadi saa sita mchana.
Anasema baada ya hapo asitafune kitu chochote, bali atumie chai na maji hadi saa mbili usiku ndipo ale, hiyo itakuwezesha kufunga kwa saa 16 na kula kwa saa nane.
Baada ya kufanya hivyo kwa wiki mbili mfululizo, anasema mtu huyo anywe chai saa sita na kula chakula saa 12 jioni, hapo atakuwa amefunga saa 18 na kula kwa saa sita.
“Mbinu hiyo itaupa mwili kutafuta akiba ya nishati kwenye kitambi, misuli na maeneo mengine ya mwili. Watu wanakula mara nyingi sana na majibu yake hupatikana kupitia magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” anasema.

Post a Comment