Wananchi Moro watakiwa kutoa ushirikiano kwa Wadadisi wa Tafiti
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka wananchi Mkoani humo hususan kwa kaya zitakazofikiwa na Wadadisi au watafiti wa zoezi hilo kutoa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha tafiti hizo za kitafiti.
Mhe. Malima ametoa wito huo Disemba 20, 2023 wakati wa mkutano wake na Waandishi wa Habari uliofanyika ofisini kwake ukiwa na lengo la kuhamasisha wananchi mkoani humo kushiriki zoezi la kitaifa tafiti za kitakwimu.
Amesema, tafiti hizo zitaisaidia Serikali katika ugawaji wa Rasilimali za Taifa, kuongeza wigo wa utoaji wa huduma za jamii, ujenzi wa miundombinu na miradi mingine ya maendeleo, hivyo, amewataka wananchi kushiriki na kutoa takwimu sahihi kwa wadadisi hususan wale watakaofikiwa kwan huo ndio utakuwz mchango wao katika kufanikisha zoezi hilo la kitaifa.
“...kushiriki tafiti kama hizi ni sehemu ya mchango wako mwananchi katika kuleta maendeleo ya Mkoa wetu na ya nchi nzima...shime wananchi tushirikiane kuyatekeleza haya...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, amezitaja tafiti hizo ambazo tayari zimeanza Novemba 2023, kuwa ni pamoja na Utafiti wa Shughuli za Kiuchumi na Kijamii ukilenga kupata idadi ya shughuli za kiuchumi na kijamii zilizopo katika sekta rasmi na Utafiti wa Kilimo wa mwaka 2022/2023 ambao lengo lake ni kufuatilia maendeleo ya Sekta ya Kilimo nchini.
Katika hatua nyingine Mhe. Adam Malima amesema utafiti wa Kilimo ni muhimu kwa Mkoa huo kwani Mkoa huo umedhamiria kuwa mfano katika mapinduzi ya Sekta ya Kilimo hapa nchini kutokana na Mkoa huo kujikita katika kilimo biashara kupitia mazao mkakati matano ya Michikichi, Parachichi, Karafuu, Kakao na Kahawa ambapo wanatarajia kuzalisha miche milioni moja kwa kila zao.

Post a Comment