Ukraine haina maisha vitani bila Marekani

 


Bila msaada wa kijeshi kutoka Marekani kuna hatari Ukraine inaweza kupoteza vita dhidi ya Urusi.

Rais Volodymyr Zelensky yuko Washington kueleza hilo, akitumai anaweza kulishawishi Bunge la Congress kupitisha msaada wa dola bilioni 60 ambao umekwama huku kukiwa na mzozo kuhusu usalama wa mpaka wa Marekani.

Siku ya Jumapili, mke wa rais wa Ukraine, Olena Zelenska, alionya Ukraine iko katika hatari bila msaada wa Marekani.

Ni Marekani, sio Ulaya, ambayo imetoa sehemu kubwa ya msaada wa kijeshi kwa Ukraine.

Ulaya sasa iko njiani kuipita Marekani katika suala la msaada wa kiuchumi kwa Ukraine. Lakini Marekani iko mbele sana katika suala la msaada wa kijeshi.

Kulingana na Taasisi ya Kiel, ambayo inafuatilia misaaada hiyo - Marekani imetoa vifaa vya kijeshi vya pauni bilioni 44. Ujerumani, mfadhili mkubwa zaidi wa Ulaya, imechangia pauni bilioni 18.

Marekani sio tu imekuwa muhimu katika kuunga mkono juhudi za vita vya Ukraine, pia imewajibika kwa kiasi kikubwa kuratibu msaada huo.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius hivi majuzi alikiri Umoja wa Ulaya hautafikia lengo lake la kuipatia Ukraine makombora milioni moja kufikia Machi mwaka ujao.

Badala yake Ulaya itatuma nchini Ukraine nusu ya kile ilichoahidi. Kwa wakati huu Ukraine inahitaji angalau makombora milioni 2.4 kwa mwaka ili kuwa na uwezo wa kuendelea na vita.

Wengi wa wanachama wa Nato barani Ulaya bado hawafikii lengo la kutumia 2% ya mapato yao ya kitaifa (Pato la Taifa) katika ulinzi, kiwango kilichowekwa karibu muongo mmoja uliopita.

Wiki hii, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Grant Shapps alisema Ulaya lazima ifanye zaidi: "Hatuwezi kuendelea kuitarajia Marekani kila mara kuiokoa Ulaya."

No comments