RC Malima ataka mafuriko Kilosa yadhibitiwe, aishukuru serikali


Kufuatia mafuriko yaliyotokea Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro Disemba 4/5 mwaka huu na kuharibu miundombinu mbalimbali ya sekta ya maji, Barabara, Umeme, kilimo Afya huku nyumba 1042 zikiharibiwa na nyumba 316 zikisombwa kabisa na maji, Serikali Mkoani Morogoro imedhamiria kuchukua hatua ya kudhibiti mafuriko hayo yanayotokea mara kwa mara Wilayani humo.

Hayo yamebainishwa Disemba 22, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa kwa watendaji wa Serikali ya kurudisha miundombinu iliyokuwa imeharibiwa na mafuriko yaliyotokea mwanzoni mwa mwezi Disemba mwaka huu.

Mhe. Malima amesema kuwa Wilaya hiyo imekuwa ikikumbwa na mafuriko ya mara kwa mara na kuharibu miundombinu, mali za wananchi wake na hata kusababisha vifo, hivyo amesema sio jambo jema kuendelea kulalamika kila yanapotokea mafuriko hayo na kutaka hatua za utafiti zaidi zifanyike ili kudhibiti mafuriko hayo.




“...hatuwezi tukawa tunalalamika sisi kila siku mafuriko...wenzetu wana utaratibu wa kuvuna maji kwa hiyo tuangalie namna ya kuyavuna haya maji yapate matumizi mengine kwa watu na hasa kwenye kilimo....” amesema Mkuu wa Mkoa Malima.

Mojawapo ya Mikakati ambayo imetaka kuuchukuliwa ni Pamoja na kuvuna maji kwa kuchimba mabwawa ambayo yatakusanya maji yatakayotumika katika shughuli nyingine za kibinadamu kama umwagiliaji na matumizi mengine ya kawaida hususan kipindi cha kiangazi.

No comments