Clatous Chota Chama, kwa vyovyote vile itakavyokuwa, ni mmoja wa wachezaji wa kigeni ambaye ameweka alama katika soka la Tanzania. Kwa zaidi ya misimu minne mfululizo, Mwamba huyu wa Lusaka amekuwa kielelezo cha mchezaji bora, mbunifu, akili kubwa na mwenye nidhamu ndani ya uwanja.

Si kwamba katika kipindi hicho hakujawahi kutokea wachezaji wengine mahiri, wawe wa ndani au nje, lakini kwa namna ya kipekee kabisa, alibaki kuwa juu yao.

Kuna mtoto mmoja wa Kinyarwanda alikuja pale Yanga, anaitwa Haruna Niyonzima. Kwa mtu anayefahamu mpira, ni ngumu kutouona uwezo wa hali ya juu miguuni mwa Cecs Fabrigas wa Kigali. Na alikuwa na misimu bora kabisa akiwa hapo kwa awamu ya kwanza.

Bahati mbaya, Yanga ilikuwa chovu, haina fedha hivyo kunyanyasika kwa kipindi kirefu mbele ya Simba iliyokuwa imempata mwekezaji, wachezaji wake wakiishi vizuri, huku wakitwaa mataji kila mwaka.

Baadaye akaja Saidoo Ntibanzokinza!

Hawa ni mafundi wa soka. Lakini si mara moja au mbili, wote kwa nyakati tofauti, waliukubali uwezo wa Chama na wakatamani siku moja kucheza pamoja naye. Vile Mungu hana choyo, maombi yao yalisikilizwa na wote wamepata kucheza naye kwa nyakati tofauti, akianza Niyonzima.

Lakini hawakuwahi, nasisitiza, hawakuwahi kumaliza ufalme wa Chama pale Msimbazi.

Na ndiyo maana kwa miaka yote ambayo Tripple C amekuwa ameshika hatamu, mchezaji yeyote mzuri wa Yanga, kipimo chake ni Chama. Kelele za kushuka kwa kiwango cha mwanasoka huyu kinapigwa zaidi na mashabiki wa Yanga na wale wa Simba kwa kutokujua, nao wameingia mkenge.

Unaweza tu kujiuliza, mtu ambaye Tanzania ameshuka kiwango kwa soka lake, anawezaje kupata namba katika timu ya Taifa ya Zambia? Yes, haanzi, lakini ile tu kuvaa jezi ya KK Elevens, ni zaidi ya ubora uwanjani.

Kwa miaka mingi mashabiki wa Yanga wametafuta namna ya kuondoa ufalme wa Chama na hadi siku za karibuni, wamejikuta wakiamini kuwa Pacome Zouzzoua ni kiboko yake!

Of course Pacome ni mchezaji mzuri, lakini unamlinganishaje na Chama? Ili aweze kuwa katika mizani ya ulinganisho, angalau acheze misimu miwili kwa kiwango hikihiki cha sasa, kwani mwenzake huu ni msimu wake wa tano kwenye chati!

Lakini pia kuna vitu ambavyo mashabiki wa mpira wanapaswa kuvijua, kwamba mpira unachezwa na umri. Huwezi kuwa na kiwango kilekile kwa miaka yote. Kadiri umri unavyokuwa mkubwa, ndivyo na spidi inavyopungua. Katika umri, Pacome hatofautiani na Chama!

Binadamu tuna hulka ya kuchoshwa, hata ikiwa ni utamu. Hatupendi kuona vitu au watu wale wale wakiwa kileleni kwa miaka yote. Tunapenda mabadiliko, hata kama mwishoni yana gharama.

 

Kuna kijana kule katika muziki wa kizazi kipya anaitwa Nasibu Abdul. Amekuja amewakuta kaka zake wameshaanza muziki, yeye akajiwekea malengo yake, akatumia makosa ya kaka zake kujiweka kitofauti. Huu ni zaidi ya mwaka wa kumi sasa amebaki kileleni.

Ameanzisha lebo inayoibua vipaji. Kuna wanamuziki walikuwa hawajulikani kabisa, lakini akawatunza, akawabrand na akatumia gharama kubwa kuwapika. Rayvanny, Lavalava, Zuchu, Harmonize ambao sasa ni mamilionea.

Amefungua kituo cha redio na televisheni, ameanzisha taasisi ya vichekesho ya Cheka Tu, amefungua kampuni ya betting, akiwa amewaajiri watanzania wengi hadi hivi sasa.

Sasa shangaa, mtu kama huyu ambaye uhalisia wa maisha yake unafahamika, badala ya kuungwa mkono, kuna watu wanamuombea mabaya ashuke, wanamtuhumu kuwa freemason, hawaamini kama ni uwezo wake, wanahisi anatumia ndumba na kadhalika.

Kwanza walianza kutafuta mtu wa kumshindanisha naye, wakalazimisha lakini wakashindwa, ndipo sasa wamebakia kumtazama kwa mlengo hasi wa kishirikina!

Nia yao wao ni ashuke tu, ikibidi afilisike kabisa, bila kujali athari zitakazowapata watu walioajiriwa naye!

 

Kuna kule Libya. Muamar Ghadaf alifanya kila kitu bora kwa nchi na watu wake. Akaligeuza jangwa kuwa ardhi yenye rutuba, akaigeuza nchi yake kuwa paradiso, akiwalipa wanandoa, serikali ikigharamia kila kitu. Hakukuwa na sababu ya Walibya kukimbilia Ulaya maana kila kitu walikipata wakiwa nyumbani.

 

Wapinzani wake wakamtengenezea majungu. Vitu vidogo vidogo vikakuzwa, Walibya wakahadaika, wakashikishwa bunduki ili wamtoe madarakani. Wakamuua. Iangalie Libya leo, wote wanajuta!

 

Hata hapa nyumbani, Nyerere alitutengenezea Tanzania moja, iliyochukia rushwa, iliyoamini binadamu wote ni sawa. Licha ya uchumi mdogo, akataka watanzania wasomeshwe bure ili baadaye wakiwa na akili wachimbe madini yaliyotapakaa nchi nzima. Wapewe matibabu bure.

 

Wapinzani wake wakasema maneno mengi ya uongo dhidi yake, haambiliki, mwizi, dikteta na kadhalika. Akaona isiwe tabu, akakaa pembeni lakini angalau akahakikisha amejenga misingi ya watu kutokaa Ikulu kama yeye.

Angalia tulipo leo, wale waliosomeshwa bure ili waisaidie nchi, leo wanajisaidia wenyewe. Kwanza walitulipisha elimu, lakini leo tunaposomeshwa bure, huduma hazifanani na shule wanazosoma watoto wao. Kumbe kwa rasilimali nyingi tulizonazo, tungeweza kuzifanya shule na vyuo vyetu viwe bora zaidi ya shule binafsi. Nchi na watu wake wamebaki masikini wa kutupwa, tukiwa na viongozi mabilionea. Watu hawasomei tena maadili ya uongozi na kuyazingatia, wanafanya madili ili wawe viongozi.

Pointi yangu inabaki palepale. Makosa ya Chama ni ufalme aliojitengenezea. Leo hata jambo la kawaida tu akilifanya, inaonekana ni ukosefu wa nidhamu. Hivi kuna mchezaji gani anafurahi kutolewa uwanjani?

Au kuna ajabu gani mchezaji kusimamishwa kwa utovu wa nidhamu? Nidhamu ya mpira siyo kutomuamkia kocha, hata kutotafsiri kwa vitendo maelekezo ya mwalimu inachukuliwa kama utovu wa nidhamu.

Kuna wachezaji wengi wanaolipwa mabilioni Ulaya wanapewa adhabu ya kuondolewa kikosini. Watu wetu wa mpira hapa wameshamuondoa Chama katika usajili.

Wale wale mashabiki wa Yanga wanaomuombea njaa, ndiyo hao hao wameanza kusema akiondolewa Simba, eti hapati nafasi Yanga!

Sasa kama huyu mchezaji amekwisha kiwango chake, kwa nini unafikiria asajiliwe na timu kubwa kama Yanga, badala angalau useme hata Singida Fountain Gate hapati namba?

Wanafahamu kwa uwezo wake, viongozi wa Yanga wanaweza kuvutiwa naye na kumsajili, ndiyo maana wanaanza jitihada mapema za kumzibia ili wafurahishe nafsi zao kwamba wamemaliza enzi zake.

Hata hivyo, anaweza akawa muda wake umeisha, lakini ukweli kwamba yeye ana nembo katika Ligi Kuu Tanzania Bara itabaki milele, wapende wasipende. Mashabiki wa Simba hawakumpenda Mayele, lakini hiyo haiwezi kuondoa ukweli juu ya kile alichokionyesha kwenye ligi yetu.

Tupunguze roho mbaya, maisha haya tunaishi halafu tunaishia!

 

No comments