Waasi wa Yemen wanaoungwa mkono na Iran waiangusha ndege ya Marekani isiyo na rubani
Waasi wa Houthi wa Yemen wameiangusha ndege ya kijeshi ya Marekani isiyo na rubani, maafisa wa Marekani na vuguvugu la Houthi linaloungwa mkono na Iran wamesema.
Afisa wa Marekani alisema ndege isiyo na rubani ya MQ9 ilidunguliwa katika pwani ya Yemen na vikosi vya Houthi.
Hayo yamethibitishwa na msemaji wa jeshi la Houthi.
Hilo linawadia wakati Washington iko katika tahadhari kwa shughuli za makundi yanayoungwa mkono na Iran Mashariki ya Kati wakati mshirika wake wa karibu Israel - mpinzani mkali wa Tehran - anapambana na Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Mwezi uliopita, meli ya kivita ya jeshi la wanamaji la Marekani ilinasa makombora na ndege kadhaa zisizo na rubani zilizorushwa na Wahouthi kutoka Yemen kuelekea Israel.
Marekani imehamisha mali za kijeshi, zikiwemo za kubeba ndege, Wanamaji na meli za usaidizi, hadi Mashariki ya Kati kutokana na mvutano wa kikanda unaozingira vita vya Israel na Gaza.
Hii ni pamoja na wanajeshi kuwekwa kwenye meli za kijeshi katika Bahari Nyekundu, ambayo iko kati ya Yemen na Israeli.
Waasi wa Houthi wa Yemen wanaungwa mkono na Iran, na wamekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu na serikali rasmi ya Yemen - inayoungwa mkono na mpinzani mwingine wa Iran, Saudi Arabia - tangu 2014.
Naibu kiongozi wa kundi jingine linaloungwa mkono na Iran katika eneo hilo, Hezbollah ya Lebanon, aliiambia BBC wiki hii kwamba mauaji ya Israel dhidi ya raia huko Gaza yanahatarisha vita zaidi katika Mashariki ya Kati.
Sheikh Naim Qassem alisema kwamba "maendeleo makubwa sana na hatari yanaweza kutokeakatika eneo hilo, na hakuna mtu ambaye angeweza kuzuia athari hizo".
Wakati huo huo, Marekani pia ilisema Jumatano kwamba ilifanya mashambulizi dhidi ya kituo kimoja mashariki mwa Syria ambacho ilisema kinatumiwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na makundi tanzu.
Afisa wa Pentagon alisema mashambulizi hayo ambayo ni ya pili katika wiki za hivi karibuni yanajibu mashambulizi dhidi ya vikosi vya Marekani nchini Iraq na Syria.
Shirika la uchunguzi wa vita vya Syrian Observatory for Human Rights limesema kuwa shambulizi hilo limeua watu tisa wenye mafungamano na makundi yanayoungwa mkono na Iran nchini Syria, takwimu ambazo haziwezi kuthibitishwa kivyake.

Post a Comment