UN yasema mtuhumiwa wa mauaji ya Kimbari Rwanda alifariki miaka 25 iliyopita
Umoja wa Mataifa umethibitisha kifo cha Aloys Ndimbati, mtuhumiwa mauji aliyesakwa sana kwa uhalifu wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 alifariki miaka 25 iliyopita.
Katika taarifa yake, kitengo kinachoshughulikia kesi zilizoachwa na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda mjini Arusha (ICTR), kinasema kuwa Aloys Ndimbati alifariki dunia mwishoni mwa Juni mwaka 1997.
Kitengo hicho kinasema kwamba ilichukua miaka hiyo yote ya mashauri kabla ya kufikia uamuzi kuwa alifariki.
Ndimbati alishtakiwa kwa makosa saba ya mauaji ya halaiki, uhalifu ambao inasemekana aliufanya katika manispaa ya Gisovu, ambako alikuwa mbabe wakati wa mauaji ya kimbari.
Kulingana na kitengo hicho, Ndimbati alifariki mwishoni mwa Juni mwaka 1997,katika kijiji cha Gatore katika wilaya ya Kirehe jimbo la Mashariki mwa Rwanda.
Taarifa Zaidi zinasema kwamba alikuwa amerejea mwezi Jun imwaka 1997 kutoka Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), ambako alikuwa amekimbia na familia yake mwezi Julai ,1994, baada ya mauaji ya kimbari.
Hata hivyo, tangu alipowasili katika kijiji cha Gatore, hakuna taarifa zozote kumhusu zilizojulikana, isipokuwa uchunguzi wa Umoja wa Mataifa unathibitisha kwamba hakuondoka mahali hapo.
Kutokana na hali yamtafaruku uliokuwepo wakati huo, taarifa hiyo inasema kuwa haikufahamika ni kwa namna gani Aloys Ndimbati alifariki.
Shirika la Umoja wa Mataifa, hata hivyo, linasema kuwa kifo hicho kimethibitishwa na ofisi ya mashtaka ya Rwanda katika uchunguzi wake.
Wakati wa mauaji ya kimbari, Aloys Ndimbati alikuwa mkuu wa wilaya ya Gisovu katika mkoa wa zamani wa Kibuye. Hapo ndipo inasemekana aliamuru mauaji ya Watutsi.
BBC

Post a Comment