KAMATI YA SIASA MKOA WA PWANI YAKAGUA MIRADI YA MAENDELEO WILAYANI BAGAMOUO
Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Pwani chini ya Mwenyekiti wake ndugu Mwinshehe Mlao leo *tarehe 16/11/2023* imeanza ziara ya kukagua miradi ya Utekelezaji wa Ilani Katika Mkoa huo.
Ziara hiyo imeanzia katika Wilaya ya Bagamoyo ambapo Kamati hiyo ya Siasa iliweza kukagua miradi minne ya Ujenzi wa Shule mpya ya awali na Msingi Kiembeni ambayo imejengwa kwa fedha za Boost huku ikiwa na Jengo la Utawala, vyumba vya madarasa elimu ya Msingi 14, madarasa 2 ya mfano ya elimu ya awali, Matundu ya vyoo vya wanafunzi wa elimu ya Msingi 16 pia Matundu 6 ya elimu ya awali na Matundu 2 ya vyoo vya waalimu na kichomea taka.
Pia Kamati hiyo ilipata wasaa wa kukagua ujenzi wa mradi wa jengo la wagonjwa wa dharura ( EMD ) katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo ambalo limejengwa kwa jumla ya fedha shilingi 300,000,000.00 kutoka Serikali Kuu ikiwa ni fedha za UVICO 19.
Aidha mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na tayari jengo hilo limeanza kutumika mpaka sasa jumla ya wagonjwa 34 tayari wameshapatiwa huduma za dharura. Jengo hilo linatarajiwa kuhudumia wagonjwa wa dharura ikiwemo waliopata ajali zaidi ya 45 kwa wakati mmoja.
Katika ziara hiyo Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Pwani imekagua shule mpya ya Msingi ijulikanayo kwa jina la Ridhiwani Kikwete iliyoko Chalinze yenye madarasa 16, jengo la Utawala na Matundu 24 ya vyoo.
Shule hiyo imejengwa kwa muda wa miezi minne huku ikigharimu jumla ya shilingi 468,694,342/= mpaka kukamilika kwa asilimia 100 na kusajiliwa kwa namba *EM. 20161* tangu tarehe *12/10/2023* na inatarajiwa kupokea jumla ya wanafunzi 760 ( wasichana 380 na wavulana 360 ).
Baadaye Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Pwani imeweza kutembelea na kukagua mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka JNHPP hadi Chalinze na kituo Cha kupoza umeme Cha Chalinze.
Mradi huo unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100 huku gharama za mradi huo mpaka kukamilika ni shilingi bilioni 128 Hadi sasa umefikia asilimia 86.23 .
Malengo ya mradi huo ni kuwa na mashineumba sita (6) zenye ukubwa wa 250 MVA Kila Moja sawa na MVA 1,500 kwa ujumla ambazo zitaboresha upatikanaji wa umeme kwenye Gridi ya Taifa na kuongeza hali ya ubora na uhakika wa upatikanaji wa umeme katika Gridi ya Taifa kwa kuunganisha umeme wa JNHPP kupitia kituo Cha kupoza umeme Cha Chalinze.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani NDG *Mwinshehe Mlao* amemshukuru Mhe, Dk. Samia Suluhu Hassan Raisi wa Jammhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwa wananchi wa Jimbo la Chalinze na Bagamoyo ambazo zimekuwa majibu ya kero zao.
Ndg Mlao amesema fedha hizo zimeleta suluhisho la changamoto zilizokuwa zikiikabili huduma ya afya katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo na kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule za Msingi Kiyaraka na Bwilingu ambapo zimepatikana shule mbili mpya kupitia mradi wa BOOST.
Amewataka waalimu kufundisha kwa bidii ili waache alama ya matokeo mazuri ya ufaulu mkubwa yatakayoleta tija kwa Bagamoyo, Chalinze na Taifa kwa ujumla.
Aidha aliwapongeza Wabunge wa Majimbo ya Bagamoyo Mhe Muhalami Mkenge na Chalinze Mhe Ridhiwani Kikwete, Wakurugenzi na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kwa usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo unaoipa CCM kutembea kifua mbele.
Alimalizia kwa kuwataka watumishi wa Halmashauri zote mbili kuendelea kuwa waaminifu na waadilifu kwa kutunza kile kinachopatikana kupitia mapato ya ndani.
Akizungumzia Utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo *Bi Halima* *Okashi* amesema mpaka sasa tayari asilimia 98 ya ILANI imetekelezwa wilayani humo.
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo *Mhe* *Muhalami Mkenge* ameiomba CCM Mkoa wa Pwani kusaidia upatikanaji wa majengo yanayomilikiwa na Hospitali ya Muhimbili yaliyoko karibu na Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo ili yawe sehemu ya Hospitali hiyo katika kuwahudumia wananchi wa Jimbo hilo.
Katika kuhitimisha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze *Mhe. Hassan* *Mwinyikndo* alikishukuru Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Pwani kwa ushirikiano wao wanaouonesha kwa Halmashauri hiyo katika kufanikisha Utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM.
Ndg Mwinyikondo alimalizia kwa kuahidi kuendeleza uaminifu na uadilifu kwa fedha za maendeleo ya miradi ya Serikali ili malengo ya CCM yatimie.
Imeandaliwa na:
David Mramba
Katibu wa Siasa na Uenezi
Mkoa wa Pwani.

Post a Comment