Baba wa mchezaji wa Liverpool, Luis Diaz bado asakwa na wanajeshi Colombia
Msako mkubwa wa jeshi na polisi unaendelea nchini Colombia kumtafuta baba yake mshambuliaji wa Liverpool Luis Diaz, huku mamlaka ikitenga zawadi ya pauni 40,000 (zaidi ya shilingi milioni 100) kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa za kumuwezesha kumuokoa.
Zaidi ya wanajeshi 120, pamoja na polisi, walimtafuta Luis Manuel Diaz kaskazini mwa Colombia siku ya Jumapili, huku kukiwa na ripoti kuwa watu waliokuwa na silaha walikuwa wamemchukua yeye na mke wake.
Mama yake mchezaji huyo, Cilenis Marulanda, alipatikana mjini Barrancas siku ya Jumamosi. Diaz hakuwepo katika kikosi cha Liverpool ambacho kiliishinda Nottingham Forest siku ya Jumapili.
Jeshi hilo limesema limeweka vizuizi barabarani na kupeleka vikosi viwili vya magari, ndege zisizo na rubani, helikopta na ndege yenye rada katika kumsaka baba yake.
Mamlaka ya Colombia haijatoa maelezo zaidi kuhusu utekaji nyara huo ulioripotiwa, lakini vyombo vya habari vya ndani vilisema mama na baba yake Diaz walichukuliwa na watu wenye silaha wakiwa kwenye pikipiki katika kituo cha mafuta cha Barrancas, mji wa nyumbani kwao, ulioko La Guajira, eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.
Rais wa Colombia Gustavo Petro alisema "majeshi yote ya umma yametumwa" kumtafuta babake Diaz.

Post a Comment