MBOWE, MUIGE KIJANA WAKO ZITO KWA MADAM PRESIDENT!

 

Na Ojuku Abraham

Kwa wanasiasa, baadhi ya vitendo vya Rais Samia Suluhu Hassan ni kete. Katika siasa, kila unachokifanya, kiwe kibaya au kizuri, kinachukuliwa kama fursa na wapinzani, wawe nje au ndani ya chama chako.

Siku zote mwanasiasa yupo vitani. Kwa mfumo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wapinzani wanaanzia kwenye jumuia uliyopo kama vile UVCCM, UWT na Wazazi. Ili kupata nafasi ya kuwa mbunge kwa mfano, watu wanapaswa kupambana kuanzia huko kabla ya kufika kwenye Uchaguzi Mkuu unaoshirikisha vyama vingi.

Miaka michache iliyopita, wakati wa uongozi wa Rais John Pombe Magufuli, ushindi kwa wagombea wa CCM haukuwa jambo la kuuliza. Kazi kubwa ilikuwa ni kwa mgombea kupitishwa na vikao husika vya ngazi za chama chake.

Baada ya Madam President kushika kijiti na kuleta maridhiano, ambayo kwa wananchi wa kawaida waliyahitaji sana, hali ni tofauti kabisa kwa wanasiasa, hasa wa chama chake. Wanaweza kuwa wanafurahi mbele ya kamera, lakini kiukweli, hali kwao ni ngumu sana.

Kitendo cha Rais Samia kusimamia maridhiano, maana yake kitaondoa baadhi ya vikwazo (siyo vyote) ambavyo vilikuwa vikiwazuia wanasiasa wa upinzani kupata ushindi. Ili maridhiano yaonekane yamefanyika, kuna usawa fulani lazima uonekane umewekwa kwenye uchaguzi!

Maana ya hii ni kuwa ili mtu ashinde, sasa siyo suala lile la kumtegemea msimamizi wa uchaguzi akimbie ofisini ili mgombea wa upinzani aonekane hajarudisha fomu aweze kupita bila kupingwa. Sasa inabidi mapambano ya majukwaani, mitaani na mbinu zingine.

Kwa namna Madam President na viongozi wengine wa vyama vya upinzani wanavyokwenda, ni tumaini la kila mwananchi wa kawaida kwamba uchaguzi mkuu ujao, 2025, utakuwa ni mmoja kati ya chaguzi bora kabisa zilizowahi kushuhudiwa katika Tanzania.

Bahati nyingine nzuri kwetu kama taifa ni kwamba tangu Mwalimu Nyerere alipobariki uwepo wa vyama vingi mwaka 1992, kufuatia kazi nzuri ya kura ya maoni iliyojulikana sana kama White Paper, hatujawahi kuona msuguano mkubwa wa kisiasa kiasi cha kuhatarisha amani.

Pamoja na uwepo wa ushindani mkubwa miongoni mwa wanasiasa, lakini wananchi hawajawahi kuathiriwa kwa namna ya kupoteza vitu vyao, ukosefu wa amani au hata kulazimika kukimbia makazi yao, ukiondoa wanasiasa wachache waliofanya hivyo kipindi cha miaka michache iliyopita.


Na staili ya uongozi wa Mama Samia, ni wazi kuwa nchi yetu itatuchukua miaka mingi kabla ya kushuhudia vurugu za kisiasa. Tunakwenda kujenga demokrasia inayokwenda sambamba na utamaduni wetu wa kuheshimiana.

Kama ambavyo Rais Samia amesema mara kadhaa, kuwa wapo wafahidhina ndani ya chama chake na hata upinzani, ambao hawapendezwi na maridhiano yanayoendelea kujengwa. Kwa nini hawapendi? Jibu ni rahisi tu, kwamba wao wanafikiri zaidi kuhusu matumbo yao!

Kama nilivyotangulia kusema hapo juu, moyo wa maridhiano wa Rais Samia una upinzani mkubwa kutoka kwa watu wa chama chake, kwa sababu kwa kinachotokea, ni wazi kwamba wengi watapoteza nafasi zao za kisiasa, hasa ubunge.

Kwa namna ambavyo grafu ya upinzani ilivyokuwa ikikua, kama haki ingetendeka katika uchaguzi uliopita, leo hii kungekuwa na wabunge angalau nusu kutoka vyama vya upinzani kwa pamoja.

Kuwanyima ulaji watu zaidi ya 100 siyo jambo dogo kwa watu wanaofikiria ustawi wa matumbo yao, lakini si kitu kwa wale wanaolifikiria taifa lao. Watu hao wakose kazi lakini nchi isonge mbele kwa amani, upendo na utulivu!

Ni kwa kutazama hali hiyo, ndipo unapoweza kuona ni jinsi gani Madam President alivyo adui miongoni mwa watu wa chama chake. Ni zawadi gani basi mwanamke huyu wa kwanza kushika nafasi hii anapaswa kupewa?

Zitto Zuber Kabwe ameonyesha njia. Amesema ACT Wazalendo haitasimamisha mgombea katika uchaguzi wa 2025 ili kumlipa heshima aliyowapa wapinzani, hasa kwa kile kitendo cha kukubali kukaa nao meza moja na kujadili masuala ya kitaifa!

Ni rai yangu kwa vyama vingine, hasa kile kikuu cha upinzani, Chadema. Mpeni heshima mama kwa namna alivyowaheshimu na kuiheshimisha nchi yetu. Tumuachie asimame peke yake, sisi tupambane huku kwenye ubunge.

Vyama hivi vikifanya hivyo, vitamuondolea presha na hivyo kujikita zaidi katika kuangalia namna ya kuiboresha Tume ya Uchaguzi na Katiba mpya. Hivi vitu viwili vikifanyika, kutakuwa na uwanja sawa katika uchaguzi wa 2030, ambao sasa wapinzani wanaweza kuingiza timu, lakini wakiwa tayari na mtaji wa wabunge.

NASIMAMA NA MAMA 2025!

 

 

 

 


No comments