MAZINGIRA YA BIASHARA NCHINI YAVUTIA SHIRIKA LA NDEGE LA SAUDIA
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akifafanua jambo kwa wadau wa usafiri wa Anga, (hawapo pichani) wakati wa hafla wa mapokezi ya ndege ya Shirika la Saudia iliyotua kwa mara ya kwanza katika Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere kutokea Nchini Saudia Arabia, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu itahakikisha mazingira ya biashara ya ndani na nje yanaimarishwa ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi kufanya biashara na Tanzania.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mara baada
kupokea ndege ya kwanza aina ya Airbus A320 ya
Shirika la Ndege la Saudia iliyotua kwa safari yake ya kwanza nchini
kupitia Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Waziri Prof.
Mbarawa amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha viwanja vya ndege nchini
vinatumiwa na mashirika mengi zaidi ili kuinua pato na kukuza biashara na
utalii.
Kaimu Balozi wa Saudi Arabia Nchini, Mhe. Fahad Alharbi akizungumza na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa katika hafla wa mapokezi ya ndege ya Shirika la Saudia iliyotua kwa mara ya kwanza katika Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere kutokea Nchini Saudia Arabia, jijini Dar es Salaam.
“Niwahakikishie ndugu wananchi kuwa Serikali imeamua kuifungua nchi kupitia anga lake, na kama mnavyoona mashirika ya ndege yanaendelea kuja nchini kupitia katika viwanja vyetu hii ni dalili nzuri katika kukuza pato na kuimarisha biashara kati yetu na nchi nyingine” amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesema usafiri wa anga
umeendelea kukua siku hadi siku kwani kumekuwa na ongezeko la idadi ya abiria
katika kiwanja hicho kutoka abiria milioni Moja na Laki Sita kwa mwaka 2021
hadi abiria milioni Milioni Mbili na Laki Sita kwa mwaka 2023 ongezeko ambalo
limeifungua Tanzania kibiashara na kiuchumi.
Kaimu Balozi wa Saudi Arabia Nchini, Mhe. Fahad Alharbi (kushoto) akizungumza na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Katikati) hafla wa mapokezi ya ndege ya Shirika la Saudia iliyotua kwa mara ya kwanza katika Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere kutokea Nchini Saudia Arabia, jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amesema Tanzania na Saudia Arabia zimekuwa zikifanya biashara ya nyama na mboga mboga hivyo uwepo wa safari za ndege za shirika hilo utarahisisha usafirishaji na kukuza biashara baina ya nchi hizo mbili.
Naye Kaimu Balozi wa Saudi Arabia Nchini, Mhe. Fahad Alharbi amesema Tanzania na Saudia Arabia zimekuwa na mashirikiano katika Nyanja mbalimbali hivyo kupitia usafiri wa anga mahusiano yataboreshwa zaidi kwani abiria watakuwa wakija na kuondoka kwa kutumia saa chache tofauti na zamani ambapo walilazimika kupitia maeneo mengine.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini, Mussa Mbura amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa mamlaka imejipanga kutoa huduma bora kwa mashirika yote yanayotoa huduma ya usafiri wa anga katika viwanja nchini na kuongeza kuwa TAA imejipanga kuhakikisha mpaka kufikia mwezi Juni inaongeza mashirika yanayotoa huduma.
Ndege ya Shirika la Ndege la Saudia aina ya
Airbus A320 yenye uwezo wa kubebea abiria takribani 180 imetua jijini Dar es
Salaam na itakuwa ikifanya safari zake moja kwa moja kutoka Nchini Saudi Arabia
kuja Tanzania mara 4 kwa wiki.
(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)


Post a Comment