KENYA YACHUKUA TAHADHARI UGONJWA ULOIKUMBA TANZANIA
Wizara ya afya ya Kenya imeongeza ufuatiliaji kwenye mpaka wake na Tanzania kufuatia kugunduliwa kwa Ugonjwa wa Virusi vya Marburg.
Mkurugenzi Mkuu Dk.Patrick Amoth amewashauri wananchi kutoa taarifa za ongezeko lisilo la kawaida la watu wanaougua homa kali na waliosafiri hivi karibuni nchini Tanzania.
"Watu kama hao wanashauriwa kuripoti mara moja katika kituo cha afya kilicho karibu ili kufanyiwa tathmini na uchunguzi." Dk Amoth alisema katika taarifa yake.
Mlipuko wa ugonjwa huo nchini Tanzania umeripotiwa mkoani Bukoba ambako kuna safari nyingi za watu kati ya Kisumu, magharibi mwa Kenya na eneo hilo.
Karibu watu 161 wamefuatiliwa na wanachunguzwa. Maafisa pia wanawafuatilia watu wengine.
Kati ya watu wanane waliopatikana na ugonjwa huo, watano wamekufa.
Wanne kati yao wanatoka katika familia moja.
WHO inasema ugonjwa wa Virusi vya Marburg unaua kwa wastani nusu ya walioambukizwa. Virusi hupitishwa kutoka kwa popo wa matunda na huenea kati ya wanadamu kupitia majimaji ya mwili.
Ingawa hakuna chanjo au matibabu, wale wanaogunduliwa nayo hupewa maji kwa mdomo au kwa njia ya mishipa kwani madaktari hutibu dalili maalum za mgonjwa.

Post a Comment