KAMATI YAITAKA TANROADS KUZINGATIA VIPENGELE VYA GHARAMA KWENYE MIRADI

Na Mwandishi Wetu

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuhakikisha wanaingia mikataba ya ujenzi yenye gharama isiyokuwa na nyongeza za fedha.

Imesema wakandarasi wengi  wanaoingia mikataba ya ujenzi na Tanroads wanakuja na mfumo wa nyongeza za gharama hali inayoisababishia serikali gharama zisizokuwa na tija.


Mwenyekiti wa kamati hiyo, Seleman Kakoso alitoa maagizo hayo jana jijini Dar es Salaam wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua ujenzi wa miundombinu ya mradi wa Dart awamu ya pili eneo la Mbagala.

"Serikali imetoa fedha nyingi katika ujenzi wa mradi huu. Jitihada ni nzuri zimefanyika, tumeridhika na kwa sasa kuna maendeleo. Lakini igeni mfumo wa TRC katika ujenzi wa barabara. Wakandarasi wanakuja na mfumo wa nyongeza za gharama hali inayosababisha miradi kuwa na gharama kubwa," alisema Kakoso.


Mbali na kutoa agizo hilo, kamati hiyo iliagiza Tanroads wanapojenga Miundombinu wazingatie uelekeo ya maji kutotiririka kuelekea kwa wananchi.Pia Tanroads wanapaswa kuimarisha ulinzi katika maeneo ya chini ya madaraja pamoja na mikataba wanayoingia imalizike kwa wakati na kusiwepo na nyongeza ya muda.



Kadhalika, kamati hiyo ilitoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanaitunza miradi ya serikali ili kuleta maendeleo endelevu.Akizungumza baada ya maagizo hayo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema wameyapokea maagizo hayo na watayafanyia kazi.Profesa Mbarawa alisema kuhusu mfumo wa nyongeza ya gharama kwa wakandarasi watakwenda kujifunza kwa TRC.

No comments