BOTSWANA YAKANUSHA KULA NJAMA KUMUUA KIONGOZI WAKE WA ZAMANI
Serikali ya Botswana imepuuzilia
mbali madai kwamba inapanga kumkamata na kumuua rais wa zamani aliye uhamishoni
Ian Khama iwapo atarejea nyumbani.
Katika mahojiano wiki iliyopita, Khama aliliambia shirika la
habari la AFP kwamba alikuwa na taarifa kuhusu mipango ya kumkamata na kumtia
sumu alipofika nyumbani kutoka Afrika Kusini, ambako amefukuzwa tangu 2021.
Alidai serikali ya Botswana inahofia ushawishi wake kabla ya
uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Lakini katika taarifa yake siku ya Jumanne, Katibu Mkuu wa
mawasiliano William Sentshebeng alipuuzilia mbali madai ya Khama na kusema ni ‘ya
kukasirisha na ya kusikitisha.’
"Tunayachukulia madai hayo kuwa yamechochewa kisiasa na kwa
nia moja tu ya kuchafua sifa nzuri ya Botswana na serikali yake," Bw
Sentshebeng alisema.
Huku uchaguzi ukikaribia mwaka ujao, Khama ameapa kumng'oa
mrithi wake Mokgweetsi Masisi, ambaye sasa ni mpinzani mkubwa anayemtuhumu kuwa
tishio kwa demokrasia.
Khama alisema anajiandaa kurejea nyumbani kujiunga na vyama
vingine ili kuhakikisha kwamba kiongozi wa sasa na chama chake wanashindwa
katika uchaguzi.
Kiongozi huyo wa zamani alisema amefanyiwa uchunguzi kamili wa
matibabu na kusasisha wosia wake kwa sababu alikuwa na uhakika kwamba ndani ya
siku chache baada ya kuwasili atakamatwa.
Khama mwenye umri wa miaka 70, afisa mkuu wa zamani wa kijeshi,
alitawala mojawapo ya mataifa ya juu zaidi barani Afrika yanayozalisha almasi
kwa muongo mmoja hadi 2018, kabla ya kukabidhi enzi kwa Masisi, ambaye wakati
huo alikuwa naibu wake.
Mzozo kati yake na mrithi wake ulianza 2018 wakati Rais Masisi
alipoanza kubadili baadhi ya sera kuu zilizopitishwa wakati wa uongozi wa Bw
Khama.
Mnamo Januari, Rais Masisi alitia saini makubaliano ya
maridhiano lakini ushindani kati ya wawili hao unaendelea.
Mnamo Disemba mwaka jana, Botswana ilitoa hati ya kukamatwa kwa
Bw Khama, kwa madai ya kumiliki silaha kinyume cha sheria.


Post a Comment