TAMESA WAJIBU MSHANGAO KIVUKO KILICHONUNULIWA KWA BIL.9 KUKARABATIWA KWA BIL.7.5

Siku moja baada ya Serikali kumtangaza mkandarasi atayekifanyia ukarabati kivuko cha MV Magogoni na kuleta mshangao na maswali mengi kwa wananchi, Wakala wa Ujenzi na Umeme Tanzania (TAMESA) imetoa ufafanuzi kwa umma.

Juzi, TAMESA ilisema imeingia mkataba na Kampuni ya African Marine and General Engineering Company Ltd ya Mombasa, kukifanyia ukarabati kivuko hicho kwa gharama ya shilingi bilioni 7.5.

Serikali ilinunua kivuko hicho mwaka 2008 kwa gharama ya shilingi bilioni 9.2.

Baada ya taarifa hizo, wadau walipiga kelele sana mitandaoni, wakisema kulikuwa na ufisadi wa wazi, kwani haiwezekani bei ya ukarabati ikawa karibu na ya ununuzi.

TAMESA, kupitia Kitengo chao cha Masoko na Uhusiano, imetoa ufafanuzi wa suala hilo.



Kimesema kivuko hicho kilichojengwa na Kampuni ya Kijerumani ya Neuer Ruhrorter Schiffswert mwaka 2008, kiligharimu kiasi cha Euro ( Fedha za Ulaya) 5, 572,000 ambazo kwa viwango vya kubadilisha fedha za kigeni wakati huo, Euro moja ilikuwa sawa na shilingi 1,758.78, ilikuwa ni sawa na shilingi za Kitanzania 9, 289, 501, 384.

Lakini kikasema wakati ukarabati ukifanyika mwaka 2023, miaka 13 baadaye, viwango vya kubadilisha fedha za kigeni vimebadilika, kwani hivi sasa Euro moja ni sawa na shilingi 2, 487.786 ambapo ukarabati huo utagharimu kiasi cha Euro milioni 3 na ushee, ambazo kwa fedha za Tanzania ni kiasi cha bilioni 7.5.

Kitengo hicho kikaendelea kusema kuwa endapo serikali ingetaka kununua kivuko chenye uwezo kama huo, wa tani 500, sawa na abiria 2000, kungeigharimu kiasi cha shilingi bilioni 25 kwa sasa.

Gharama hizo za bilioni 7.5, kitengo kimesema kinatokana na kuagiza nje vifaa vyote vitakavyotumika katika ukarabati huo, usafirishaji wa chombo hicho kutoka Dar es Salaam kwenda Mombasa na kurudi, ukaguzi kikiwa Mombasa na kadhalika.

No comments