SIMBA NA YANGA ZOTE ZINAWEZA KUSHINDA MECHI ZAO BENJAMIN MKAPA
Simba na Yanga zinazialika timu kubwa zaidi yao Barani Afrika katika michuano inayosimamiwa na Shirikisho la Soka (CAF).
Simba inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, inaikaribisha Raja Cansablanca ya Morocco wakati Yanga, wawakilishi wa nchi katika Kombe la Shirikisho, watakuwa wenyeji wa TP Mazembe kutoka DRC.
Ni mechi ngumu kwa wawakilishi hawa wa Tanzania, kwa kama ambavyo namba huwa hazidanganyi, hata uwezo wa mchezaji mmoja mmoja una tofauti kubwa kati ya timu hizo za nje na za kwetu.
Ni kweli Simba na Yanga za sasa siyo zile za zamani, zimebadilika kila kitu, kuanzia uendeshaji, aina ya wachezaji, maisha ya wachezaji wake na hata ushirikiano kati ya timu na mashabiki.
Hivi sasa kuna uwekezaji umefanywa katika timu hizi, watu wameweka fedha zao, tena nyingi kwa viwango vya Tanzania. Soka sasa ni utajiri na vijana wanafahamu.
Kuna wachezaji wengi wa kigeni katika timu hizi, wakitokea Zambia, Burundi, DRC, Uganda, Kenya, Mali, Burkinafaso, Nigeria na hadi Senegal.
Hata hivyo, tunapowalinganisha wachezaji wa kigeni wanaochezea timu zetu na wale wa timu pinzani, ipo tofauti kubwa.
Hata TP Mazembe inachukua wachezaji kutoka nchi ambazo timu zetu zinachukua, lakini tofauti ni viwango. Wao, kutokana na uchumi wao kuwa mkubwa, wanachukua wachezaji bora zaidi yetu.
Raja kwa mfano, inachukua wachezaji wengi kutoka ukanda wa Afrika Kaskazini, ambao ni bora kuliko ukanda mwingine wowote Afrika.
Ni wazi, vita vitakavyopiganwa leo na kesho pale Benjamin Mkapa, ni kati ya Daudi na Goliati.
Simba imewahi kushinda mechi nyingi dhidi ya timu kutoka Afrika Kaskazini zinapocheza ardhi ya Tanzania, lakini kama ambavyo wote tunajua, usbindi wa mechi haubadili ukweli wa ubora.
Yanga hali kadhalika, wamewahi kuzishinda timu nyingi bora Afrika wakicheza nyumbani, lakini hilo halimaanisbi kuwa Wananchi ni bora.
Wakati timu zetu hizi zikianza kuingia katika ubora, kiuhalisia, mechi hizo kimahesabu, tunafungwa, ila kihistoria tunao uwezo wa kushinda.
Tutashinda kwa sababu tunacheza katika ardhi yetu, nyuma ya mashabiki wetu na muhimu zaidi, tunao wachezaji wenye uwezo binafsi wa kuamua baadhi ya vitu kwa manufaa ya timu.
Binafsi, sitashangaa Simba na Yanga zikipoteza nyumbani, lakini nafahamu tunao uwezo wa kushinda kwa sababu tutacheza tukiwa na joto la mama, milioni tano kwa kila bao ni nyongeza ya hamasa.
Mungu zibariki Yanga na Simba!!

Post a Comment