RUVUMA KUTUMIA MIEZI MITATU KUWAPANGA MACHINGA MAENEO RASMI
NA STEPHANO MANGO, SONGEA
UTEKELEZAJI wa mapitio ya
mpango wa upangaji wajasiriamali wadogo (Machinga) katika maeneo rasmi ya
kufanyia biashara, mkoani Ruvuma utafanyika kwa kipindi cha siku tisini.
Haya yamesemwa na Mkuu wa
Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakati anataja
maazimio kwenye kikao cha mkakati wa kuwapanga Machinga katika maeneo ya
kufanyia biashara kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Kikao hicho
kimeshirikisha wadau kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma
wakiwemo wakuu wa wilaya, wenyeviti wa Halmashauri, makatibu Tawala, Kamati ya
ulinzi Mkoa wa Ruvuma, viongozi wa Machinga ngazi ya Mkoa, wakurugenzi wa
Halmashauri, wataalam mbalimbali na viongozi mbalimbali wa Taasisi za serikali
zikiwemo TRA, SOUWASA, TANROADS, TARURA,RUWASA na LATRA.
Brigedia Jenerali Ibuge
amekitaja kipindi cha utekelezaji mkakati huo kuwa ni kuanzia Mwezi Novemba, Desemba
na Januari 2022 na kwamba wameazimia ifikapo Januari 30 mwakani
utekelezaji wa kuwapanga Machinga uwe umekamilika.
“Ili kuhakikisha zoezi
hilo linafanikiwa kwa weledi, tunaazimia itakapofika Novemba 30, majadiliano ya
uboreshaji kwa kuzingatia uwakilishi wa makundi yote yakiwemo viongozi wa
Machinga yatakuwa yamekamilika hivyo tutakutana tena hapa kama wadau ili kupata
mrejesho’’,alisisitiza RC Ibuge.
Ameagiza zoezi la
upangaji maeneo lishirikishe viongozi waliochaguliwa na Machinga kwenye maeneo
yao ili kuleta umoja na ushirikishwaji katika makundi yote.
Hata hivyo
ametahadharisha kuwa uboreshaji wa mpango wa upangaji Machinga, pale ambapo
utawahusisha wafanyabiashara wakubwa wasiokuwa Machinga, ni lazima kuhusisha
vikao vya pamoja nao ili kutoingia mwenye migogoro.
Mkuu wa Mkoa ameagiza
Halmashauri zote nane mkoani Ruvuma kuhakikisha kuwa, baada ya makubaliano, waweke
miundombinu wezeshi kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya Machinga ili kuweza
kwenda sanjari na mwisho wa utekelezaji wa kuwapanga Machinga kwenye maeneo
yao.
Ameziagiza Taasisi zote
kwenye Halmashauri zikiwemo TRA, TARURA, RUWASA, TANESCO, TANROADS na LATRA
washiriki kikamilifu kuwezesha maeneo muhimu ya kuwekewa miundombinu
wezeshi ili kuwezesha uhamaji na upangaji wa Machinga katika maeneo
rasmi ya biashara.
Hata hivyo amesisitiza
kuwa kutokana na upekee wa zoezi la upangaji Machinga, juhudi za makusudi
zifanyike kuhakikisha mabaraza ya Biashara ya Halmashauri na Manispaa yawe
yamepata taarifa na kufanya majadiliano ya utekelezaji wa mpango wa Halmashauri
husika na viongozi wa Machinga kabla ya kikao cha marejeo.
RC Ibuge ameutaja
upangaji wa Machinga kwenye maeneo rasmi kwa Mkoa wa Ruvuma kuwa ni fursa kubwa
kwa kuwa Halmashauri zina maeneo makubwa ambayo yanatakiwa kuwekewa miundombinu
kwa ajili ya kuwawezesha Machinga kufanya biashara bila shida.
Akizungumza kwenye kikao
hicho Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Ruvuma Salum Masamaki ameishukuru
serikali kwa kuwapangia Machinga maeneo rasmi ya kufanyia biashara
ambapo amesema sasa wataweza kufanya biashara zao kwenye maeneo yenye utulivu
na kwamba wapo tayari kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa zoezi hilo.
Naye Mwenyekiti wa CCM
Mkoa wa Ruvuma Ndugu Odo Mwisho ameipongeza serikali kwa kutoa fursa ya
kuwapangia Machinga maeneo rasmi ya biashara ambapo ametoa rai kwa viongozi wa
Machinga Mkoa kuzunguka katika Wilaya zote ili kutoa elimu kwa
Machinga kuhusu mpango huo wa serikali wenye tija kwao.
Mkuu wa Wilaya ya
Nyasa Kanali Laban Thomas akizungumza kwenye kikao hicho
ametoa rai kwa Machinga kuondoa hofu kwenye utekelezaji wa mpango
huo ambapo amesisitiza Machinga wana thamani kubwa kwa sababu popote
watakapopangiwa na serikali, wanunuzi watafuata bidhaa zao.
Pololet Mgema ni Mkuu wa
Wilaya ya Songea ametoa rai kwa viongozi wa Machinga Mkoa wa Ruvuma, kufuatilia
muundo wa Taasisi yao yenye viongozi kuanzia ngazi ya kitaifa, ili kujua katiba
yao inavyoelekeza ili kutekeleza majukumu yao kwa maslahi
ya Machinga wote.
Mkoa wa Ruvuma
unakadiriwa kuwa na wajasiriamali wadogo (Machinga) wapatao 28,000 ambao
wanafanya biashara zao kwenye maeneo mbalimbali ya Halmashauri nane za Mkoa.

Post a Comment