TMA YAONYA UKAME, JUA KALI NCHINI
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania
(TMA) imesema kuna uwezekano mkubwa wa kutokea kwa ukame kutokana na upungufu wa
mvua unaotarajiwa kutokea katika kipindi cha mvua za vuli zinazotarajiwa kuanza
kunyesha hivi karibuni.
Imebainishwa kuwa katika kipindi cha mvua za Oktoba hadi
Desemba mikoa mingi itakuwa na upungufu mkubwa wa mvua ambazo zitakuwa chini ya
wastani hadi wastani na pia kunatarajiwa kuwepo kwa vipindi vya joto kali
lisilo la kawaida.
TMA imetoa tahadhari hiyo jana wakati wa utabiri wa mvua za
Vuli, ambazo ni mahsusi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini zinazotarajiwa
kuanza kwa kusuasua katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Oktoba 2021 ikiwa na
mtawanyiko na muendelezo usioridhisha katika maeneo mengi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Huduma za
Utabiri wa TMA, Dk. Hamza Kabelwa amesema mifumo ya hali ya hewa inaonyesha
mvua za Vuli zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani na zinatarajiwa
kuambatana na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi yanayopata mvua za
Vuli.
Amesema hali hii itapekeleka kutokea kwa athari mbali mbali
zitakazotokana na hali ya ukavu kwa maeneo yatakayokosa mvua ikiwemo upungufu
wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi na
kutokeza kwa magonjwa ya mlipuko, kutokana na upungufu wa maji safi na salama.
Athari zingine ni uwezekano wa kujitokeza upungufu wa malisho
na maji hivyo kusababisha kujitokeza kwa migogoro kati ya wafugaji na watumiaji
wengine wa ardhi.
Uwezekano wa kutokea matukio ya moto katika mapori na misitu,
hivyo mamlaka husika zinashauriwa kupanga mikakati mahsusi ya kukabiliana na
hali hiyo.
Amesema, msimu wa mvua za Vuli ni mahsusi kwa maeneo ya
nyanda za juu kaskazini mashariki, mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro na
Pwani ya kaskazini, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani ikijumuisha
visiwa vya Mafia, Dar es Salaam na Tanga, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Katika ukanda wa Ziwa Victoria, Mikoa ya Kagera, Geita,
Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma wilaya
za Kibondo na Kakonko.
"Kutokana na mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwa sasa na
inavyotarajiwa katika kipindi chote cha msimu kwa ujumla mvua za chini ya
wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu
miwili ya mvua kwa mwaka" amesema Kabelwa.
Amesema, baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria
yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Aidha Mamlaka TMA, imetoa ushauri katika sekta mbalimbali
ikiwemo Kilimo, usalama wa Chakula , Mifugo na Uvuvi, Utalii na Wanyamapori, Usafiri
na Usafirishaji, Nishati , Maji na Madini, Mamlaka za Mji, Sekta ya Afya , Sekta
binafsi pamoja na Menejimenti za Maafa kuhakikisha zinachukua tahadhari za
mapema ili kuweza kuepukana na majanga yoyote yanayoweza kujitokeza katika
kipindi huu hicho cha mvua chache.
Pia wameshauriwa kuendelea kufuatilia utabiri unaotolewa na
wataalamu mbalimbali kipindi chote cha Mvua za Vuli.
Chanzo Michuzi Blog

Post a Comment