MSAJILI WA VYAMA AITAKA CHADEMA KUWEKA PICHA YA RAIS KWENYE OFISI YAKE
MSAJILI Msaidizi wa Vyama vya
Siasa, Sisty Nyahoza ameishauri Chadema kuweka picha ya Rais katika ofisi za
viongozi wa chama hicho kwa sababu hiyo ni taasisi ya umma.
Ushauri huo umetolewa leo Ijumaa Septemba 10, 2021
wakati wakifanya ukaguzi wa chama hicho katika utekelezaji wa Sheria ya Vyama
vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi.
Amesema ofisi za vyama vya siasa ni ofisi za umma
hivyo ni vizuri wakaendeleza utamaduni wa kuwa na picha ya Rais kwenye taasisi
za umma.
"Hii ni ofisi ya umma, ni vizuri kukawa na
picha ya Rais ukutani, siyo unaweka picha ya katibu mkuu. Huu ni ushauri
tumewapa, tutapita Januari kuona kama wamelifanyia kazi," amesema Nyahoza.
Akizungumzia suala hilo, Naibu Katibu Mkuu wa
Chadema - Zanzibar, Salum Mwalimu amesema Msajili amekuta mambo yamekaa vizuri
ndiyo maana akagundua hakuna picha ya Rais.
"Tumempokea Msajili, wamepitia taarifa zote
walizozihitaji wamekuta mambo yako vizuri, ni masuala madogo madogo ndiyo
yanahitaji kufanyiwa kazi. Kama angekuta mambo makubwa, asingekumbuka kuangalia
picha ya Rais," amesema Mwalimu.
Ofisi ya Msajili inaendelea na ukaguzi wa vyama
vya siasa na leo walikuwa wakikagua Chadema ambapo Nyahoza amesema
wamefurahishwa na mfumo mzuri wa uwekaji kumbukumbu za fedha na wana mfumo
mzuri wa utawala.
Hata hivyo, amesema wamebaini mapungufu kadhaa
ikiwemo uwekaji kumbukumbu kwenye mali za chama na pia wameanza kutumia bajeti
ambayo wameiandaa lakini haijaidhinishwa na kamati kuu kama katiba yao
inavyotaka.

Post a Comment