MIZANI WATAKIWA KUTOA ELIMU KWA WASAFIRISHAJI WAKATI WOTE
Naibu Waziri wa
Ujenzi na Uchukuzi,
Mwita Waitara, amewataka Wakala wa Barabara (TANROADS),
kukutana na wadau wa usafirishaji mara kwa mara ili kuwaelimisha Sheria ya
Udhibiti Uzito wa Magari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni
zake za mwaka 2018 zinavyofanya kazi ili
kuondoa malalamiko ya mara kwa mara.
Akikagua utendaji
kazi wa Mizani ya Nala jijini Dodoma leo, Naibu Waziri Waitara amewataka wafanyakazi
wa mizani kutoa
elimu kwa kila
dereva wa lori
kila anapokaguliwa ili kuepusha
madereva hao kuongeza
mizigo njiani na kusababisha usumbufu kwa wamiliki wa malori
na lawama kwa wafanyakazi wa mizani.
“Hakikisheni
mnapopima magari mnawaeleza uzito uliopo na ni nini anastahili dereva kufanya
ili kuepuka kuzidisha uzito na kuharibu barabara”, amesisitiza Naibu Waziri
huyo.
Akiwa katika
mizani hiyo Naibu
Waziri Waitara ameshuhudia
baadhi ya madereva wa
malori kukiri kuongeza
mizigo ya ziada
na hivyo kukamatwa kutokana na kuzidisha uzito hali
ambayo inasababisha usumbufu kwa wamiliki.
Amewataka
wasimamizi wa mizani kote nchini kuhakikisha kwamba abiria wa mabasi yaliyozidisha uzito hawapati
usumbufu wanapokuwa safarini kwa makosa ya madereva.
Aidha,
amewasisitiza watumishi wa mizani kuhusu umuhimu wa kutenda haki kwa magari yote yanayozidisha uzito ili
kuondoa malalamiko na upendeleo.
Naye, Kaimu
Meneja wa TANROADS,
Mkoa wa Dodoma,
Mhandisi Salehe Juma, amesema
magari mengi yanayotozwa
faini yanatokana na
ukaidi wa madereva wenyewe
kutotoa taarifa kwa wamiliki pindi wanapokamatwa kwa kosa la kuzidisha uzito
kwani sheria inatoa fursa kwa magari kukaa siku tatu bila ya kuchajiwa kwa
ajili ya kupunguza mizigo iliyozidi.
Naibu Waziri huyo
alikuwa kwenye ziara ya kukagua changamoto zinazoikabili Kitengo cha Mizani
ikiwa ni muendelezo wa mkakati wa Wizara kujenga taswira njema katika huduma ya
usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Post a Comment