JAMII: KWA NINI NDUGU HAWATAKIANI MEMA KULIKO WATU BAKI?

 Majonzi yatawala maziko ya ndugu watano wa familia moja - Mwananchi

NDUGU ni nani? Laweza kuwa swali gumu kama utataka kulipa tafsiri kwa upana wake, lakini kwa lugha nyepesi na ya kueleweka haraka, hapa tunamzungumzia mtu uliyezaliwa naye damu moja.

Na damu moja nayo ni tafsiri pana vilevile, lakini angalau inafahamika kuwa huenda ni jamii moja, ukoo mmoja au familia moja.

Kwa mfano, mimi simfahamu babu wa babu yangu, lakini naufahamu ukoo wetu unaoanzia kwa babu wa baba yangu. Babu huyu wa baba alizaa watoto kwa mama wanne tofauti na watoto wake hao ndiyo wakawazaa baba na shangazi zetu ambao nao walituzaa sisi ambao sasa nasi tuna watoto!

Kwa hiyo ndugu si lazima uzaliwe naye tumbo moja, mnaweza kuwa mnatoka jamii au ukoo mmoja. Lakini kuna nyakati pia hata ndugu wa tumbo moja, huombeana mabaya!

Kwa nini?

Kutokana na uzoefu wangu wa maisha ya kujichanganya na kuishi sehemu mbalimbali za nchi ambako nimekutana na watu wa namna tofauti, kitu cha dhahiri nilichogundua ni kuwa watu wachache sana wanandugu hupendana kwa dhati ya moyo.

Wengi wetu huishi na ndugu wa namna hii kwa namna ya kuviziana, kila mmoja akiombea mwenzake atende mabaya ili apate sababu ya kumsema kwa ndugu wengine.

Kwa mfano, ndugu mmoja atatangulia kuanzisha maisha mjini, tuseme Dar es Salaam na wenzake wakajua. Kwa vile tunafahamu kuwa Dar ni sehemu ya fursa, wengi watapenda kuja wakiamini wakifika watafikia kwa ndugu yao, hasa kama amefanikiwa angalau kidogo.

Ndugu atakapofika hapo, tuseme labda ni mtoto wa shangazi, mjomba, baba mdogo, baba mkubwa, mama mkubwa, mama mdogo na ye yote wa namna hiyo, atajieleza kuwa amekuja mjini japo apate kibarua chochote cha kufanya ambacho kitaweza kumsaidia kupata fedha kwa ajili yake na ikibidi kwa ajili ya ndugu zake wengine aliowaacha nyuma kijijini.

Kikawaida, ndugu yule wa mjini atajitahidi kutafuta fursa kwa ajili ya ndugu zake, ama kwa kuwaomba marafiki zake wamsaidie kutafuta sehemu ya kujishikiza au kama ana shughuli zake, basi atamuweka amsaidie huku akimlipa kidogo.

Kwa mfano ndugu akiwa na duka, genge, shamba au gereji, atamuweka huyo nduguye. Hapo kuna kuviziana baina yao, kila mmoja anamuomba Mungu nduguye akosee. Yule aliyemkaribisha, ataombea mwenzake aharibu kazi ili apate sababu ya kumfukuza au kumsimanga na aliyesaidiwa atasubiri asimangwe bila kosa ili apate sababu.

Ikitokea wamekwaruzana, kila mmoja atakimbilia kwa ndugu na kulalamika. Huyu kanifanya hivi, yule kanifanya hivi, ili mradi kila mmoja atajaribu kuonyesha jinsi ambavyo nduguye asivyo mtu mzuri.

Pamoja na kwamba binadamu tumezaliwa kila mmoja na karma yake, lakini kiasili, kila mmoja anayo dhambi ya asili, UBINAFSI. Sisi hasa waswahili, ni wabinafsi tunaopenda mambo mazuri yawe kwetu tu na si kwa wenzetu.

Ingawa ni kweli kuwa wapo baadhi ya ndugu zetu wenye upendo na sisi kwa kiwango kikubwa, hata kama wao wamefanikiwa, lakini dhambi hii haiwachepuki.

Binadamu tuna hulka ya kupenda sifa. Tukiwa katika nafasi ya kusifiwa, hatupendi mwingine pia awe na sifa kama yetu, yetu tunataka iwe spesho, kubwa na nzuri kuliko za wenzetu.

Katika familia kwa mfano, aliyefanikiwa hupenda abaki yeye peke yake ili ndugu wote waende kwake kulia shida, anaamini endapo ndugu mwingine atapata uwezo wa kuwasaidia wengine kama afanyavyo yeye, hatapata sifa anazozipata hivi sasa.

Hii ndiyo sababu kubwa ya kuombeana mabaya. Ikitokea kwenye familia wamefanikiwa wawili, wataanza kupigana vijembe, kila mmoja akitaka aonekane bora kuliko mwenzake mbele ya familia yao, jambo ambalo kimsingi, linakosa mbolea.

Ukichunguza familia nyingi zilizokuwa bora huko nyuma kutokana na kufanikiwa kwa mmoja wao, leo zimejaa ufukara kwa sababu aliyefanikiwa hakutaka kutengeneza mafanikio kwa wenzake, aling'ang'ania kubaki peke yake ili aonekane ndiye Mungu wa familia.

Sasa angalia familia zile ambazo mmoja aliyefanikiwa, aliwavuta na kuwawezesha wenzake nao kupata mafanikio. Maisha yao yameendelea kuwa bora kwa sababu katika matatizo, badala ya wote kumtegemea mtu mmoja, sasa wanashirkiana kulikabili tatizo, kiasi kwamba hata mchango wao huonekana mdogo kwa kuangalia mafanikio yao.

Mtu, yaasi sisi waswahili, hata akipata 'mchongo' wa hela nyingi kwa mfano, yupo tayari kumpa mtu baki kuliko ndugu yake. Anaamini ndugu yake akipata mchongo kisha akapata fedha nyingi, atajidai na kumdharau.

Lakini je, dhana hii ina ukweli kiasi gani? Zipo baadhi ya nyakati zinathibitisha kuwa ndugu wengi waliokuja kufanikiwa kupitia kubebwa na ndugu, baadaye waligeuka na kuwa maadui. Wakati mwingine hata kudai waliowasaidia wanawaonea wivu.

Ingawa pia ni kweli kwamba baadhi ya ndugu waliowapokea wenzao hapa mjini, wakiona waliyemsaidia amefanikiwa, huanza kumtafuta kwa maneno ya chinichini, ili mradi tu kuonyesha bila wao, huyo mtu asingepata mafanikio aliyopata.

Makosa yote haya husababisha chuki baina ya ndugu na hivyo kuzalisha dhana mpya iliyowakaa watu wengi kwamba ni heri umsaidie mtu baki atakuheshimu kuliko ndugu.

Hata hivyo, kitu kimoja cha msingi ambacho wote tunapaswa kukielewa ni kuwa kiasili, wote tuna ubinafsi. Hii ni dhambi ya kuzaliwa nayo, kila mtu anayo. Leo hii tutamlilia ndugu yetu aliyetangulia mbele za haki na wengine hujikuta hata wakisema Mungu ni bora ungenichukua mimi ungemuacha yeye!

Lakini kama Mungu angekuwa anataka kututenda, angeweza kuibuka na kutushika mikono kwamba twende badala ya marehemu, hakika wengi wangekimbia.

Kuishi na dhambi hii, haikufanyi uwe na roho mbaya kwa ndugu yako. Kuna ule msemo usemao tenda wema nenda zako. Usitoe kwa mategemeo ya kulipwa, wewe timiza jukumu lako, matokeo anayajua Mungu.

Ninaamini kama kuna mtu mmoja amefanikiwa kwenye familia, akimuwezesha mmoja naye akafanikiwa, wawili hawa wana uwezo wa kuwawezesha wenzao kiasi kwamba baada ya miaka michache, ndugu wote mtakuwa na uwezo wa kuweza kusaidiana.

Utataka sifa kwa kuwa ndiye uliyefanikiwa peke yako, lakini unasahau jinsi unavyorudi nyuma kimaendeleo kwa sababu shida zote za familia au ukoo unalazimika kuzitatua wewe peke yako.

Hii inaenda hadi kwa wazazi, baba ni tajiri kwa miaka mingi, lakini akifa tu na mali zinaanza kukimbia, kwa nini? Baba hakutaka kuwafundisha watoto namna ya kutafuta na kulinda mali tangu akiwa hai, angewafundisha na kuwasimamia, leo hii wasingeyumba!

 

 


No comments