WABUNGE WATAKA MWENZAO ALIYETOLEWA NJE KISA MAVAZI AOMBWE RADHI

SAKATA la kutolewa nje kwa mbunge wa Momba, Condester Sichwale (CCM) kuhusu mavazi yaliyosemwa kuwa yasiyo na staha, limeibuka tena jana jioni katika kikao cha Bunge baada ya wabunge wanawake kutaka aombwe radhi na aliyetoa hoja.
Hata hivyo mbunge Hussein Amar amesema hawezi kuomba radhi
kwa sababu alichosema alikuwa sahihi kwa kuwa mavazi aliyovaa mbunge mwenzake
hayakuwa na staha ndiyo maana Spika wa Bunge Job Ndugai aliridhia hoja
aliyoitoa yeye (Amar).
Katika kikao cha jana jioni wabunge Jacqueline Ngonyani na
Stella Manyanya waliomba mwongozo wa Spika kwa madai mbunge aliyetolewa nje
alionewa.
Mapema jana Sichwale alitolewa nje kwa amri ya Spika baada ya
Amar kuomba mwongozo kwa kutumia kanuni 170 kuhusu mavazi ya staha.
Ngonyani amesema kilichotokea ni kwamba mbunge huyo alionewa
kwani alikuwa na vazi la staha ambalo halikuwa na shida lakini akasema huenda
Spika hakuona.
"Mimi ni mjumbe wa Baraza Kuu la wanawake wa CCM,
ninapoona kuna uonevu lazima niseme na hili sikiungi mkono huyu mwanamke
mwenzetu ameonewa,"amesema Ngonyani.
Mbunge huyo amesisitiza kuwa uonevu wa namna hiyo haupaswi
kuvumiliwa kwa kuwa umemdhalilisha mbunge huyo na wapiga kura wake jimboni.
Kwa upande wake Manyanya amesema tangu asubuhi alikuwa
anafuatilia kwenye mitandao na amebaini kuwa Sichwale hakuwa na vazi baya.
Hata hivyo Manyanya amesema haiwezekani wabunge vijana wavae
mavazi kama wanayovaa wabunge wanawake watu wazima.
Amesema katika siku za karibuni limeibuka suala la kutoa
lugha za kuwadhalilisha wabunge wanawake ndani ya ukumbi ambako wakati mwingine
hutamkwa kiungo cha mwanamke halafu wengine wanafurahi.
Naibu Spika Dkt. Tulia Akson amesema atatoa mwongozo baada ya
kufuatilia jambo hilo.

Post a Comment