UGONJWA WA NGURUWE WAINGIA MORO, MARUFUKU KUSAFIRISHA KITOWEO NJE YA MKOA

NGURUWE 12 wamethibitika kufa
kutokana na homa ya nguruwe Manispaa ya Morogoro na serikali imepiga marufuku
usafirishaji wa wanyama hao na nyama yake kutoka nje ya mkoa huo.
Aidha, kata tano kati ya 29 za Manispaa ya Morogoro
zimethibitika kuathiriwa na ugonjwa huo.
Ofisa Mifugo wa Manispaa ya Morogoro, Dk. Petro Lema,
alithibitisha hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuwa ugonjwa huo
hauna madhara kwa binadamu atakekula nyama ya nguruwe aliyeathiriwa.
Alisema walipata taarifa ya kuibuka kwa ugonjwa huo Juni 2 na
kuchukua sampuli kuzipeleka maabara ya chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
na kubaini kuwapo kwa vimelea vya ugonjwa huo kwa nguruwe waliokufa katika kata
za Kingolwira, Tungi, Kichangani, Boma na Kilakala.
Dk. Lema alisema uchunguzi wa awali wamebaini kuwa ugonjwa
huo kutokea mkoani Dodoma na Manispaa ya Morogoro ulianzia kata ya Kingolwira
na idara ya mifugo kwa kushirikiana na jeshi la polisi tayari wameshaweka
vizuizi katika mpaka wa barabara ya Iringa, Dodoma na Dar es salaam ili kuzuia
wafanyabiashara kuingiza au kutoa wanyama hao.
Alisema wanaokula nyama hiyo kwenye vibanda, mabucha na baa
hawaruhusiwi kubeba mabaki kupelekea mifugo nyumbani ili kuepuka ugonjwa huo
kusambaa.
“Tumeendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali wakiwamo
wauzaji wa kitoweo cha nguruwe, wafugaji na wauzaji chakula cha mifugo, ugonjwa
huu unasababishwa na kirusi na hautibiki,” alisema.
Pia, alisema atakayekiuka masharti atachukuliwa hatua ikiwamo
kutozwa faini ya Sh. 200,000 na watakaobainika kuwa na nyama hiyo bila mihuri,
nyama itateketezwa.

Post a Comment