SUGU, MSIGWA WAFUNGUA KESI YA KIKATIBA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA

WABUNGE wa zamani wa Majimbo ya
Iringa Mjini, Peter Msigwa na Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi wamefungua kesi ya
kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kile walichosema haki na utu wa
wafungwa wawapo jela.
Miongoni mwa madai yao ni pamoja na wafungwa kulazimishwa kuvuliwa nguo ili
kukaguliwa na kupimwa ukimwi kwa lazima na matokeo kutangazwa hadharani.
TAARIFA KWA VOMBO VYA HABARI
Ndugu Wanahabari,
Tunapenda kutoa taarifa hii muhimu kwenu, ili mtusaidie kusambaza kwa wananchi
lengo kuu likiwa ni sehemu ya uchechemuzi juu ya Haki za Msingi ambazo ziko
ndani ya katiba na ambazo ni stahili ya kila raia wa Tanzania.
Sisi Mchungaji Peter Msigwa na Mheshimiwa Joseph Mbilinyi ambao tulikuwa
wabunge wa majimbo ya Iringa Mjini Na Mbeya Mjini, tumefungua kesi ya kikatiba
katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Kuu Ya Dar es salaam dhidi ya
Mwanasheria mkuu wa serikali na Kamishna wa Magereza Tanzania tukipinga
kukiukwa kwa haki zetu za msingi na za kikatiba wakati tunatumikia adhabu
tulizopewa na mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Mbeya.
Labda kwa kifupi kwa wale ambao hawakumbuki, mimi Mheshimiwa Peter Msigwa na
viongozi wenzangu tulikuwa tunakabiliwa na kesi ya Jinai Namba …….ya Mwaka 2019
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Baada ya kukamilika kwa kesi hiyo
Tarehe 10 Mwezi Machi Mwaka 2020 tulipatikana na hatia na kutakiwa kulipa faini
ya TZS 40,000,000/= au kutumikia kifungo cha miezi mitano (5) jela. Hatukuweza
kulipa kiasi hicho kwa wakati, kitu kilichopelekea kutumia kifungo jela mpaka
pale kiasi hicho kilipopatikana ambapo tulilipa faini hiyo na kuachiwa huru.
Kwa upande wa Mwenzangu Joseph Mbilinyi yeye alikuwa anakabiliwa na kesi ya
Jinai katika mahakama ya hakimu mkazi Mbeya ambapo alipatikana na hatia na
kuhukumiwa kifungo cha miezi sita (6) bila faini. Mwenzagu alitumikia kifungo
mpaka alipopata msamaha wa jumla wa rais Tarehe 26 Mwezi 4 Mwaka 2018.
Kwa minajili hiyo kufungua kesi hii ya kikatiba kunatokana na kukiukwa dhidi
yetu kwa haki zetu za kikatiba na za msingi katika kipindi ambacho tulikuwa
tunatumikia adhabu zetu.
Baada ya hapo tuseme kuwa nchi yetu anaendeshwa na Katiba amabayo ndio sheria
Mama, Sura ya kwanza, sehemu ya Tatu ya katiba yetu inaanza na ibara 12 na
kumalizikia ibara 32, sehemu hii ndio ambayo inabainisha Haki na wajibu Muhimu
wa wananchi na vile vile inatoa fursa chini ya Ibara 30(3) kwa mtu yoyoyte
kufungua shauri Mahakama Kuu endapo ataona kuwa haki yake imevunjwa.
Labda tueleze pia kuwa Nchi yetu sio kisiwa kwa hali hiyo katika nyanja ya
mahusiano ya kikanda na kimataifa nchi yetu imesaini na kuridhia mikataba
kadhaa kuhusu haki za msingi za wananchi wake hii ikiwa ni pamoja na Tamko la
Haki za Binadamu, mkataba wa Afrika juu ya haki za watu na mkataba wa kimataifa
wa haki za kiraia na kisiasa.
Nyaraka hizo nne zilizotajwa zinaeleza bayana pamoja na haki nyingine haki za
msingi zifuatazo:
KATIBA YA JAMBURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MWAKA 1977 KAMA ILIVYOREKEBISHWA
IBARA YA 12 (1) na (2)
(1) Binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa.
(2) Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.
- IBARA YA 13 (6)
Kwa madhumuni ya kuhakikisha
usawa mbele ya sheria, Mamlaka ya Nchi itaweka taratibu zinazofaa au
zinazozingatia misingi kwamba–
wakati haki na wajibu wa mtu yeyote vinahitaji kufanyiwa uamuzi wa mahakama au
chombo kinginecho kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa
ya kusikilizwa kwa ukamilifu, na pia haki ya kukata rufaa au kupata nafuu
nyingine ya kisheria kutokana na maamuzi ya mahakama au chombo hicho kinginecho
kinachohusika;
(b) ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu
mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo;
(e) ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu
zinazomtweza au kumdhalilisha.
- IBARA YA 14 :
- Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata
kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sharia
- IBARA YA 16
- Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata
hifadhi kwa nafsi yake binafsi na familia yake na unyumba wake, na pia
heshima na hifadhi ya maisha yake na mawasiliano yake ya binafsi
- IBARA YA 18
- (1) Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila
mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta,
kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya
kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa kutoingiliwa kati mawasiliano yake.
- IBARA YA 19
- Kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa
mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa mtu
kubadilisha dini au imani yake.
7. IBARA YA 23(1) NA (2)
1) Kila mtu, bila ya kuwapo ubaguzi wa aina yoyote, anayo haki ya kupata ujira
unaolingana na kazi yake, na watu wote wanaofanya kazi kulingana na uwezo wao
watapata malipo kulingana na kiasi na sifa za kazi wanayoifanya.
2) Kila mtu anayefanya kazi anastahili kupata malipo ya haki.
Ibara za katiba tulizozitaja hapo juu kwa namna moja au nyingine zipo pia
kwenye mikataba kadhaa ya haki za binadamu ambayo tumesaini na kuridhia
matumizi yake. Mikataba hiyo ni Mkataba wa haki za binadamu wa Afrika, tamko la
Haki za Bianadamu na mkataba wa haki za kisiasa na Kiraia. Ibara ya 9(f) ya
katiba inatamka bayana kuwa mamlaka ya nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika
kuelekeza sera na shughuli zake katika lengo la kuhakikisha kwamba heshima ya
binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata kanuni za Tangazo la dunia
kuhusu Haki wa Binadamu.
Katika kipindi chote ambacho tulikuwa gerezani kutumikia adhabu tulizopewa na
mahakama kulikuwa na ukiukwaji mkubwa sana wa haki za msingi kama inavyoanishwa
katika katiba yetu na Katika mikataba kadhaa ambayo nchii hii imetia sahihi,
katika vifungu vilivyo orodheshwa hapo juu.
Mifano halisi ya ukiukwaji huo ni:
- Kushindwa kutambua utu wa wafungwa: ndugu
wanahabari katika kitu kinachodhalilisha utu wa mtu gerezani ni kitendo
cha kuambiwa kuvua nguo mbele ya hadhara kwa ajili ya upekuzi wa mwili.
Utaratibu unaotumika ni wa kizamani na wa kinyama sana ambao hauzingatii
umri wa mtu na faragha ya mtu. Huu ni utaratibu unaotweza na kudhalilisha
binadamu.
- Kulazimishwa kupimwa UKIMWI na kupewa
majibu mbele ya hadhara na bila kufuata masharti ya kitabibu yanayohitaji
vipimo viwe kwa ridhaa na majibu kutolewa kwa siri.
- Utaratibu wa kutoa adhabu gerezani
hauzingatii kabisa kanuni ya msingi ya haki ya kusikilizwa
- Kitendo cha kuwafanyisha kazi wafungwa
bila kuwalipa kutokana na kazi wanazofanya
- Utaratibu wa jeshi la magereza kuwapa
wafungwa sare moja anapoingia bila kuwa na sare ya kubadili endapo sare
imechafuka na anataka kuisafisha.
- Utaratibu wa kuwalazimishwa wafungwa
kutotumia sehemu za haja kubwa pasipo kupata ruhusa na askari magereza na
kitendo cha kuweka ni mara ngapi kwa siku mfungwa anatakiwa kutumia sehemu
za haja
- Utaratibu wa kuwapa madaraka maafisa
magereza kuwaadhibu wafungwa bila kuwapa wafungwa hao haki ya kusikilizwa
- Kuwa na utaratibu wa kutoa adhabu za
viboko kwa wafungwa wanaokutwa na hatia ni adhabu ambayo ni ya
kudhalilisha na kutweza utu wa binadamu na hasa kwa namna ambavyo adhabu
hiyo inapaswa kutekelezwa kwa mujibu wa sheria na kanunu za magereza.
- Kutoa adhabu ya kumyima mfungwa na au
kumpunguzia chakula ni ukiukwaji mkubwa wa haki ya kuishi.
- Kutoa adhabu ya kumfungia mfungwa peke
yake kwa muda Fulani kwenye chumba maalumu (solitary confinement).
- Kujaza wafungwa wengi na kuwalaza kwenye
chumba kimoja na kutokuwapa nguo maalumu ya kutumia wakati wa kulala kwa
mfano mashuka na mablanketi ni hatari kwa afya wa wafungwa hata katika
kipindi hiki dunia inapitia katika changamoto ya janga la COVID19
- Kuwalazimishwa wafungwa kunyoa nywee zao
na kubaki na vipara bila kujali Imani za dini za wafungwa.
- Kutokuwa na utaratibu wa kuwapa fursa
wafungwa kukata rufaa pale wanapokutwa na makossa chini ya utaratibu wa
adhabu kwaa wafungwa magerezani.
Tumalize kwa kusisistiza kuwa
kitendo cha mtu kupewa adhabu ya kutumikia kifungo gerezani hakina maana ya
kuondoa utu wake aliopewa na Mwenyezi Mungu, kitu pekee anachotakiwa kukikosa
ni uhuru wake na kuzuiliwa kwenda atakapo. Haki zake zingine zote
zilizoainishwa na sheria na mikataba ya kimataifa zinaendelea kuwepo na inabidi
zilindwe na kuheshimiwa kama amabavyo mtu amabaye sio mfungwa anapata.
Pamoja na kuwa anatumikia adhabu lakini kuzuiwa kwake kukosa uhuru wake
unatakiwa uchukuliwe kwa njia za kistaarabu (The least intrusive and reasonable
measures what would achieve the objective).
Katika jicho la sheria mfungwa si mnyama bali ni biadamu kama binadamu wengine
wowote. Haki zake zote za kisheria na kikatiba ni lazima zilindwe na
ziheshimiwe, utu wake usitwezwe na kudharauliwa na hatikiwi kupewa adhabu za
kikakatili na za kudhalilisha utu, na wala hatakiwi kuteswa kiakili na kimwili
kwani kufanya hivyo ni sawa na kumuadhibu mara mbili kwa kosa moja.
Chini ya sheria za haki za binadamu kama zilivyoainishwa hapo juu ikiwemo
katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, serikali ina wajibu wa kulinda na
kuheshimu haki za msingi za binadamu. Jukumu hili linajumuisha serikali
kutokuvunja haki hizo lakini pia kuchukua hatua pale ambapo haki hizo
zimevunjwa na watu wengine na kuhakikisha kwamba wahanga wanapata afua
mbalimbali. Kwa vile jukumu la kulinda Haki zetu za kikatiba lipo kwa mahakama
chini ya Ibara 30(3) na kwa vile tuna haki na wajibu wa kulinda katiba chini ya
ibara 26(2) ya katiba yetu ndio maana sisi tumeamua kupiga hodi mahakamani kutaka
mahakama kutamka kwamba vitendo vinavyolalamikiwa ni kinyume na missing ya haki
za binadamu na vinavunja katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuielekeza
serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani na Idara ya Magereza kufanya
maboresho yenye lengo la kuhakikisha kwamba haki za msingi za binadamu kwa
wafungwa na mahabusu zinazingatiwa wakiwa magerezani.
Wafungwa ni kama binadamu wengine, wasidhalilishwe, kutwezwa na kuteswa.

Post a Comment