KATIBU MKUU UJENZI AITAKA TEMESA KURUDISHA IMANI KWA WATEJA
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Joseph K. Malongo katikati akikata utepe kuzindua rasmi vitendea kazi vipya vya
karakana na viti maalumu vya walemavu katika hafla fupi iliyofanyika katika
karakana ya TEMESA Mkoa wa Dodoma leo. Kushoto kwake ni Mtendaji Mkuu wa Wakala
wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle na kulia kwake ni
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala huo Profesa Idrissa B. Mshoro. Vifaa hivyo vimegharimu kiasi cha shilingi milioni 765,512,400 vitagawiwa katika Mikoa ya kikanda; Mikoa ya
Arusha, Mwanza, Mtwara, Mbeya, Tabora na Dodoma.
Na Alfred Mgweno
KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Joseph K.
Malongo ameutaka Wakala wa
Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) kuhakikisha unakuja na mkakati maalumu ili kurudisha
imani ya wateja ambao ni watumiaji wa huduma za Wakala huo ambao ni taasisi za Serikali
na Umma.
Mhandisi Malongo ameyasema hayo mapema leo
wakati akizindua rasmi vitendea kazi vipya vya karakana
na viti maalumu vya walemavu katika hafla fupi iliyofanyika katika karakana ya
TEMESA Mkoa wa Dodoma.
Wakala umenunua Viti Maalum vya Walemavu thelathini na tatu (33) kwa
ajili ya kusaidia abiria walemavu wanaovuka katika Vivuko vya Serikali. Vifaa
hivi vimegharimu Serikali kiasi cha Tsh
765,512,400 kati ya fedha hizi kiasi
cha Tsh 494,814,900 zimetumika
kununua Karakana zinazohamishika, Tsh 257,205,780 zimegharamia manunuzi
ya Diagnostic Machine na Sinograph na Tsh
13,491,720 Viti Maalum vya Walemavu.
‘’Tunatakiwa tuje na mkakati maalumu, ‘Turn around strategy’, masoko tunayo,
uhakika wa soko tunao ambao umehakikishwa na sheria inayotulinda, magari na
mitambo elfu kumi na tano watoa huduma wengine hawana, lakini nyie mnayo,
njoeni na mkakati tuangalie tunawezaje kurudisha Imani ya wateja wetu na wateja
wetu ni Serikali,’ alisema Mhandisi. Malongo ambapo aliongeza kuwa mkakati huo
ndio utakaoonyesha njia ambayo Wakala huo utaelekea mara baada ya kuutekeleza
kwa usahihi.
‘’Niwapongeze kwa hatua nzuri ya kwanza ya kusogeza huduma karibu na
wateja wetu, na ni matumaini yangu kwamba vifaa hivi ambavyo vimenunuliwa kwa
pesa nyingi za serikali vitaenda kutumika vizuri kwa mahala husika."
Awali akizungumza katika
hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet
Y. Maselle amesema ununuzi wa karakana zinazohamishika (Mobile Workshops) umelenga kusogeza
huduma kwa wateja walio mbali na karakana za Mikoa na pili ni kutoa
huduma ya matengenezo ya dharura yanayotokea maeneo yasiyo na karakana hasa
magari na mitambo yanapokuwa safarini au kazini nje ya ofisi.
Aidha aliongeza kuwa karakana za Wilaya
zilizo mbali na karakana za Mikoa zitaendelea kujengwa
kadri ya upatikanaji wa fedha ikiwa ni pamoja na Karakana
zinazohamishika.
Mhandisi Maselle amesema
kuwa Vifaa vya kuchunguza ubovu na hitalafu za magari na mitambo (Diagnostic
Machines) viko thelasini (30) kwa lengo la kila kituo kuwa na machine yake.
‘’Wakala unaamini kubaini
tatizo kwa usahihi na kwa muda mfupi kutaboresha ubora wa huduma na kupunguza
muda wa matengenezo ya magari na mitambo. Vilevile katika kupunguza malalamiko
ya wateja kufungiwa vipuri visivyo halisia, Wakala umenunua viweka alama kwenye
vipuri (Sinograph) vitakavyotumika kwenye matengenezo ya magari na mitambo
katika karakana za TEMESA zote’’.
Karakana hizi zinazotembea zitagawiwa katika Mikoa
ya kikanda; Mikoa ya Arusha, Mwanza, Mtwara, Mbeya, Tabora na Dodoma. Katika
mwaka wa fedha 2021/22, Wizara kupitia Wakala imetenga fedha kwa ajili
ya kununua Karakana za aina hii zingine sita (6).

Post a Comment