JAMBAZI LAUAWA NA POLISI SHINYANGA


Dailynews

JESHI la Polisi Mkoani Shinyanga limemuua mtuhumiwa wa ujambazi aliyejulikana kwa majina ya Idd Masasi (43) Mkazi wa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga na Kigamboni jijini Dar es Salaam, kwa kumpiga risasi wakati wa majibizano ya risasi na askari hao wakimtuhumu kuhusika na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba amesema kuwa Mei 30, 2021 jeshi hilo lilipata taarifa za siri za uwepo wa jambazi (Idd Masasi) ambaye alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha hasa matukio yaliyotokea hivi karibuni Kigamboni, Dar es Salaam yenye namba KGD/IR/1050/2021 na KGD/IR/411/2021, ambapo taarifa hizo za siri zilieleza kuwa jambazi huyo alikimbilia mkoani Shinyanga baada ya kutenda matukio hayo jijini Dar es Salaam.

Taarifa hizo za siri pia zilibainisha kuwa hivi karibuni mtuhumiwa anapenda kutembelea maeneo ya soko la Nguzo Nane lililopo kata ya Kambarage mjini Shinyanga kwa ajili ya kusoma maeneo ya kutenda uharifu ikizingatiwa kuwa eneo hilo lina wafanyabiashara mbalimbali.

Aidha pia kumbukumbu zinaonyesha kuwa mtuhumiwa huyo alishawahi kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha mwaka 2011 na kutumikia adhabu hiyo katika gereza la Butimba, Mwanza na baadae alitoka kwa rufaa.

ACP Magiligimba amesema kuwa mtuhumiwa huyo wa ujambazi alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitalini ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

No comments