HERSI HAIJUI HADHI YA YANGA


Kikwete: Yanga SC must involve fans to make transformation a success |  Goal.com

 NILIPATA nafasi ya kusikiliza sehemu ya mahojiano kati ya Mkurugenzi wa Uwekezaji kutoka kampuni ya GSM, Injinia Hersi Said na kituo cha redio cha Efm katika kipindi cha Sports HQ.

Hersi pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga. Alialikwa katika kipindi hicho akiwa kama kiongozi wa klabu hiyo. Mambo mengi aliyoulizwa alitoa ufafanuzi mzuri sana, akiongezea hata kuelelzea baadhi ya vitu ambavyo mashabiki wa kawaida ndani ya timu hiyo, pamoja na watu wengine walikuwa hawajui.

Mambo hayo ni pamoja na muundo wa klabu baada ya mageuzi makubwa yanayotarajiwa kufanyika, endapo wanachama wataridhia katika mkutano wao unaotarajiwa kufanyika Juni 27 mwaka huu.

Lakini kuna swali aliulizwa ambalo majibu yake binafsi kama mdau wa soka, sikutegemea kama yangetoka kwa mtu anayehubiri mambo makubwa kiasi hicho kwa klabu hiyo yenye mashabiki wengi zaidi Tanzania.

Hili ni swali ambalo kila mwandishi anayefuatilia mwenendo wa soka letu na siasa zake, asingesita kuuliza, once amekutana na Hersi. Aliwaahidi wanayanga kuwa endapo timu yao itakosa ubingwa msimu huu, waulizwe wao (viongozi, na hasa GSM), je kwa mwenendo wa lLigi Kuu hadi sasa, anaonaje kuhusiana na kauli yake hiyo?

"Tayari tumeshachukua ubingwa mmoja, tena mbele ya mtani, Kombe la Mapinduzi. Tuna matumaini ya kutwaa taji la Ligi Kuu na tupo Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho, bado tuna nafasi ya kutwaa mataji. Tuna uhakika wa kulitwaa hilo kombe, mshindi kati ya Azam na Simba tukikutana naye lazima tumfunge."

Kwangu, Yanga bado ina nafasi ya kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu (ingawa kwa asilimia ndogo mno) na ule wa FA nafasi kwao ipo, kama ambavyo klabu zote zilizofikia hatua ya Nusu Fainali zinayo. Yanga, Simba, Azam na Biashara wote wana nafasi sawa ya kutwaa taji hili.

Lakini ambacho sijakielewa kwa Hersi ni kulitaja Kombe la Mapinduzi. Kwanza siamini kama aliposema Yanga ikikosa ubingwa msimu huu waulizwe wao, alimaanisha makombe mengine zaidi ya lile la Ligi Kuu. Hakika, hadi hapo itakavyokuwa vinginevyo, ninaamini mamia ya mashabiki wa soka kote nchini waliamini alimaanisha VPL!

Silidharau Kombe la Mapinduzi, ni kombe lenye hadhi kutokana na umuhimu wa siku hiyo kwa wananchi wa Tanzania. Lakini tunapokuja kumaanisha katika soka la ushindani ndani ya nchi hii, michuano ile ni kama bonanza tu, kama ambavyo huko nyuma tumewahi kuwa na michuano kama ya CCM Cup, Jengo Cup, Hedex Cup na mengineyo.

Mshindi wa michuano hii haendi popote katika michuano ya kimataifa. Unapokuwa kiongozi wa timu kama Yanga, unapozungumza kuhusu kutwaa mataji, unamaanisha yale yatakayoifanya klabu kushiriki mashindano ya kimataifa. Kulitaja kombe la Mapinduzi kama moja ya makombe ya klabu kujivunia, ni kutofahamu hadhi ya klabu ya Yanga. Yanga ya kushangilia makombe ya Bonanza?

Katika soka la nchi hii, Yanga inajisikia fahari zaidi kuweka rekodi ya kuifunga Simba. Ushindi dhidi ya Simba una hadhi kubwa kwa Yanga kuliko kubeba Kombe la Mapinduzi!

Pengine alikuwa anajaribu kulifanya suala la kukosa ubingwa wa Ligi Kuu lionekane dogo, la kawaida, kwani kama ubingwa tayari wanao!

Ninajua mashabiki wa kweli wa soka, wakiwemo wengi wa Yanga, wanaamini timu yao haiwezi kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

 

No comments