HECHE: MDEE, BULAYA NJOONI HADHARANI, MSITUME WATU

VUGUVUGU la kuhoji uhalali wa
ubunge wao tangu kufariki kwa Rais John Magufuli likiwa limepamba moto, Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche
amewataka wabunge 19 wa viti maalum waliokuwa wanachama wa chama hicho waliopo
bungeni, kujitokeza hadharani kuomba radhi badala ya kuwatumia watu kuwaombea
msamaha.
Heche ametoa kauli hiyo leo jana mjini Tarime, alipokuwa akizungumza na
wanachama wa Chadema katika mkutano wao wa ndani.
Amesema wamepata taarifa kutoka kwa baadhi ya watu ambao wametumwa na wabunge
hao kuwaombea msamaha, jambo ambalo halikubaliki.
Akifafanua, alisema wabunge hao wanapaswa kutambua kuwa chama hicho sio timu ya
mpira wala bendi ya kutoa burudani, isipokuwa kina nia ya kubadilisha maisha ya
Watanzania kutoka katika umasikini na kuishi maisha mazuri kulingana na
rasilimali zilizopo.
“Hawa wasituletee maigizo hapa na watambue kuwa hawana umaarufu kuliko watu
kama kina Zitto Kabwe na Dk. Slaa ambao baada ya kuona wanataka kutuzamisha
tuliwatosa sisi tukasonga mbele,” amesema Heche.
Amesema kama yupo mbunge mwenye nia ya kuendelea kuwa mwanachama wa chama
hicho, ajitokeze hadharani aombe radhi ili wanachama na uongozi uweze kupima
kama anastahili kusamehewa ama la.
Amesema Chadema hakijasahau usaliti uliofanywa na wao ambao walishuhudia mateso
waliyoyapata hasa wakati wa uchaguzi, ambapo baadhi ya watu walipoteza maisha
mbele zao lakini walipoambiwa chama hakikubaliani na matokeo ya uchaguzi, wao
walijitenga na kuwasaliti.
“ Hawa ndugu zetu walishuhudia magumu tuliyopitia, mfano mimi siku ya kufunga
kampeni pale Nyamongo, kuna watu walipoteza maisha baada ya mkutano wangu
kuvamiwa na polisi na kuanza kurusha risasi hovyo na haya yote hawa wenzetu
wanayajua kwa undani. Kwa sababu walikuwa ni wajumbe wa kamati kuu lakini
waliamua kuangalia maslahi yao binafsi na kuwasahau watu waliojeruhiwa, wengine
kupoteza maisha kwa sababu yao,” amesema Heche.
Amesema Chadema bado haijabadilisha dhamira yake ya kubadili maisha ya watu
kutoka hali ya unyonge na umasikini, ambayo inatumiwa na wapinzani wao
kuendelea kuwatawala Watanzania.
Amesema nia hiyo itafanikiwa kwa kutumia rasilimali zilizopo endapo tu chama
kitapata ridhaa ya kuongoza dola.

Post a Comment