USIOGOPE KUKOSEA, USIJILAUMU

KUNA nyakati, maisha yanakufikisha katika eneo ambalo unaamini hakuna namna ya kutoka na kwamba huo ndiyo mwisho wa safari yako.
Kufanikiwa kuna tafsiri nyingi sana na kila mtu anayo anavyoamini, ingawa wengi wanatofautiana viwango vya hayo mafanikio.
Kwa mfano, mwanafunzi akiwa darasani na akitambua uwezo wake, atakuambia yeye akifanikiwa tu kufaulu na kusonga mbele, akiwa la saba atapenda aende sekondari, akiwa sekondari atapenda aende form six, akiwa form six atapenda aende chuo. Kuna mwanafunzi mwenye ndoto hizo.
Lakini katika ngazi hiyohiyo, yupo mwanafunzi anayetaka afaulu kwa kupata daraja A tena la alama za juu kabisa.
Hata huku kwenye kazi zetu za kila
siku. Kuna mtu akishaajiriwa pale alipo, ameshamaliza. Kwake yeye cha muhimu ni
kazi ambayo inampatia mshahara ili afanye vitu vingine. Lakini wapo
walioridhika na pale alipo, siku zote anapenda asogee mbele zaidi, iwe kielimu,
kikazi na hata kiwadhifa.
Kitu cha msingi ninachotaka kusema, kila mmoja ana ndoto zake. Kuna sehemu mtu akifika, kwake inamtosha. Usije ukamuona mtu wa namna hiyo, ukampuuza maana hujui alipotoka.
Katika kuifikia ndoto, kuna changamoto nyingi sana, zinazotokana na mazingira, tabia nchi, watu wanaokusaidia kuifikia ndoto (Hawa ni wale ambao lazima ukutane nao, wawe wabaya au wazuri), hali halisi na wakati mwingine, makosa yako mwenyewe.
Kama una ndoto za kuwa mkulima mwenye kujiweza, inategemea na mazao unayotaka kulima, ambayo pia yataamua eneo muafaka. Kilimo ni ajira nzuri, lakini changamoto zake za jumla ni hizo, eneo, kiasi, maji, miundombinu, mbegu, mbolea na hatimaye soko.
Wapo watu wanaoshindwa kuzifikia ndoto zao za kilimo kutokana na changamoto mbalimbali.
Wengine wanajaribu kutaka kuwa wafanyabiashara, wajenzi, watoa huduma na kadhalika.
Kuelekea kule unakotaka, makosa ni lazima yawepo. Amini, hata leo tunamzungumzia tajiri mkubwa hapa kwetu kama Bakhressa, yapo makosa, tena mengi tu aliyafanya wakati akielekea pale alipo leo.
Wengi wetu tukifanya kosa moja, tunaelekea kukata tamaa na kuanza kuhisi huenda tuna mikosi au tumelogwa. Si kweli. Usigope kufanya makosa, kwa sababu makosa ni darasa zuri sana kuelekea unakotaka.
Kwa mfano, twende kwa yule anayetaka kulima. Kwa mfano amesikia zao la tikiti maji linalipa sana, na yeye akaamua kwenda kulianzisha mradi tu analo eneo, halafu akapata mavuno kidogo. Lazima kutakuwa na sababu, labda ardhi haikuwa na rutuba, haifai kwa zao lile, tikiti linahitaji maji mengi kwa hiyo huenda ardhi hiyo haiweki maji na kadhalika.
Makosa hayo yatakusaidia kutambua ama uirutubishe ardhi, au ubadilishe mazao ama utafute eneo jingine kwa kilimo cha tikiti. Ndoto zako bado unatembea nazo.
Watu wanakosea hata kusoma. Mtu
anataka awe na elimu kubwa, lakini anafanya kosa katika kuchagua elimu
anayoimudu. Mtu anaweza akawa mzuri kwenye elimu ya ufundi umeme wa majumbani
na viwandani, lakini akaenda kutaka kusomea udaktari wa binadamu!
Unaweza kusoma kwa muda, lakini ukatambua huku siko, badilisha mwelekeo ikiwa bado mapema. Siyo mbaya ukajaribu hata fani mbili, tatu, ipo moja itakufikisha unapopataka.
Na kuna wale wanaojilaumu. Kwa mfano alitaka kusomea ufundi, lakini akaghairi na kuamua kusomea kilimo, baadaye anakuta mtu aliyeingia naye ufundi, sasa hivi yupo vizuri sana kimaisha.
Asikudanganye mtu, kujilaumu ni chembechembe hai zinazosaidia kudumaza akili yako kusonga mbele. Kama nilivyosema pale juu, usiogope.
Kuna watu tunapishana maisha huku mtaani. Kuna wengine ni wachuuzi tu wa vitu sokoni, lakini wana maisha kushinda bosi mkubwa wa ofisi ya umma. Kwanza yatupasa kutofautisha mambo, kupata kipato kikubwa pale unapofanya kazi siyo kigezo cha wewe kuwa na maisha mazuri.
Hii ina mambo mengi, wengine
wanapata pesa kubwa lakini wana matumizi makubwa, wengine wanapata pesa nyingi
lakini wana majukumu mengi. Ndiyo maana unaona kijana anauza chips anajenga
nyumba, lakini bosi anafuatwa na gari la kazini lakini bado anapanga.
Kama ulifanya kosa jana, likajirudia
leo, wala usijilaumu, endelea kupambana kwa kutumia makosa hayo kujifunza.
Wanapokwambia nyani mzee amekoswa mishale mingi, hawamaanishi kweli alikutana
na wawindaji, ukute pori alilozeekea binadamu hajawahi hata kukanyaga.
Maana yao ni kuwa kujifunza na kuona
mengi ni kujua mengi!

Post a Comment