KUNA KERO ZAIDI YA OMBAOMBA


Breaking News: RAIS MAGUFULI AMTUMBUA MKUU WA MKOA WA KATAVI AMOS MAKALA. -  YouTube

 MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam ameagiza kuondolewa mitaani kwa watanzania wanaofanya shughuli ya kuombaomba kutoka kwa wapita njia, hasa mabarabarani.

Katika kusisitiza hilo, amewataka wakuu wake wote wa wilaya kuhakikisha wanaratibu zoezi hilo na kwamba ofisi yake ipo tayari kuwasafirisha kwenda makwao.

Yes, ni jambo zuri, hasa ukizingatia jambo hilo hivi sasa linawahusisha hadi watoto wadogo ambao kimsingi walipaswa kuwa shuleni. Wazazi wanakaa pembeni, zoezi la kuomba linafanywa na watoto wadogo kabisa.

Hata hivyo, sina uhakika kama Makala amefanya utafiti wa kutosha na kujijibu baadhi ya maswali ikiwemo sababu zilizowafanya ombaomba hao waondoke huko makwao, je bado zipo? Na kama bado zipo, zitatatuliwa vipi?

Kwangu mimi, hili ni zoezi ambalo lilihitaji utafiti na muda na liwe zoezi la kitaifa, si la Dar peke yake. Maana ombaomba wapo kila mahali.

Wapo ambao kwa umri wao, ni vigumu kusema unamrudisha kwao, hawa wangetafutiwa utaratibu kama ule wa kuwapeleka kwenye makazi ya wazee ambao vipo baadhi ya vituo vinavyosimamiwa na serikali, taasisi binafsi na hata kwa wasamaria wema.

Ila hawa watoto, no way, wachukuliwe na kupelekwa makwao maana huko wana ndugu na jamaa zao, wasome!

Lakini pengine Mkuu wa Mkoa ameanza na kero ambayo haiumizi na akaziacha zinazoumiza na kukera zaidi.

Kuna hawa wapiga debe bro, wanakera. Na si tu kwa makelele yao, bali hata yale matusi yao na wizi.

Dunia inahama inatuacha tumesimama palepale. Hivi hawa wanashindikana vipi kuondolewa katika vituo vya mabasi ya daladala?

Mabasi yameandikwa yanakokwenda, abiria anajua anakokwenda, kwa nini tunaruhusu wajinga wajinga hapa kati wanaleta kero?

Basi afadhali wangekuwa wanaitia hao abiria kiustaarabu, lakini watapiga piga mabasi kwa ngumi, watatukanana kwa sauti na wakati mwingine matusi makubwa makubwa na mwisho, hao hao wanawaibia abiria!

Madereva wa daladala wanawajua kama ni wezi, lakini wanaogopa kuwaondoa kwa sababu kesi itakuwa yao. Hawa Polisi wanaoshinda kukimbizana na wachimba michanga kule mabondeni, kwa nini wasisimame vituoni kuwakamata hawa wezi?

Halafu lipo tatizo lingine. Kuna hawa wahubiri, hasa wa dini ya Kikristo. Wameanza kuvamia vituo vya daladala, wanaweka maspika yao, wanaweka sauti kubwa, eti wanahubiri neno la Mungu.

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, mimi ni Mkristo, niliyebatizwa katika Kanisa Takatifu la Roma. Hawa wahubiri ni wanafiki!

Unakwendaje kuweka kambi ya mahubiri katika kituo cha abiria wanaosafiri? Sijawahi kuwasikia wakiomba ili abiria waliopo waende salama huko wanakokwenda!

Ni nani atasikiliza neno wakati ana haraka ya kwenda kibaruani kwake au anayerejea akiwa amechoka?

Wanaweka sauti kubwa kiasi cha kulazimisha kila mtu asikilize wanachosema. Ni lini tumeanza kulazimishana kuabudu? Kwa nini suala la kuabudu haliendelei kuwa binafsi la mtu kuamua kuabudu anachokitaka? Huu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaopaswa kukemewa kwa nguvu zote.

Leo tunawaacha hawa, kesho watakuja wa dini na imani zingine nao wataweka maspika yao pale, mwisho haitaweza kuwa fujo?

Anayetoa vibali vya hawa wapiga kelele kukaa vituoni analifikiria hili? Hapana, lazima tuwe taifa lenye utaratibu, kila jambo lifanyike kwa utaratibu.

Yaani ni kama ule uamuzi wa kuwaachia wamachinga kukaa kila walipojisikia. Moja kati ya maamuzi ya ajabu kabisa kuwahi kuchukuliwa na serikali ya Tanzania. Matokeo yake ndiyo hayo, kila penye upenyo, mtu anajenga banda, anaweka bidhaa, iwe nguo, nyanya, masufuria, yaani dah!

Kama hawa wachungaji wanahitaji kuwarudisha kondoo waliopotea zizini, upo utaratibu wanaopaswa kuufuata, wapewe maeneo ya kukaa, waweke spika zao wapaze sauti, wenye kuwiwa watawafuata.

 

No comments