SITA WAHOFIA KUFA MAJI MTO RUVUMA WILAYANI NYASA


Mtumbwi - Wikipedia, kamusi elezo huru

Na Stephano Mango, Nyasa

WATU sita wa familia mbili wakazi wa kijiji cha Mipotopoto, kata ya mitomoni Wilaya Nyasa mkoani Ruvuma wanahofiwa kufa maji baada ya mtumbwi (gome) waliokuwa wakisafiria kutoka kijijini hapo kwenda mashambani ambayo yapo ng’ambo ya mto Ruvuma kuzidiwa uzito na kuzama.

Akizungumza na gazeti hili jana Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zima moto na Uokoaji Mkoani Ruvuma Mkaguzi Msaidizi Chesco Mbata alisema kuwa tukio hilo limetokea Mei 22 mwaka huu majira ya saa 12 asubuhi huko eneo la mto Ruvuma  na kusababisha maafa hayo.

Kaimu Kamanda Mbata aliwataja watu hao ambao wanahofia kufa maji kuwa ni Yusuph Ummy (28) Fitina Salum(22) Fahim Ummy (2) Tosha Salum Kalomba(30) Emran Mohamed Chiponda(1) na Rambo Mohamed Chiponda(6)

Alisema kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio watu hao wa familia mbili walikuwa wakitokea nyumbani kwao na kwenda katika  shughuli zao za kilimo kwa kutumia usafiri wa kienyeji wa mtumbwi maarufu kwa jina la gome na kwamba walipofika katikati ya mto mtumbwi ulizidiwa na kasi ya mawimbi ya maji na kusababisha mtumbwi huo kupoteza muelekeo na kuzama majini.

Alifafanua zaidi kuwa baada ya kupokea taarifa hizo kutoka katika uongozi wa kijiji cha Mitomoni kupitia Jeshi la Polisi Wilayani Nyasa, askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ngazi ya Wilaya na Mkoa walifika eneo la tukio ambako waliwakuta wananchi wakiendelea kuwatafuta watu hao waliozama.

Alisema kuwa katika juhudi za uokoaji mtu mmoja ambaye amefahamika kwa jina la Emran Mohamed Chiponda(1) alipatikana na kukimbizwa katika Kituo cha Afya cha Liparamba ambako baadae alifariki dunia wakati anaendelea kupatiwa matibabu.

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Isabela Chilumba alipohojiwa na blog hii, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi ambao wanazunguka ziwa Nyasa na mito mikubwa yote iliyopo wilayani humo kuchukua tahadhari  wanapovuka mito hiyo kwani imekuwa na mawimbi na kasi kubwa ya maji.

Kwa Upande wake kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Simon Maigwa alisema kuwa jitihada za uokoaji zinaendelea na kutoa wito kwa wananchi kuacha kutumia chelezo aina ya gome katika kuvuka mito mikubwa kwa usalama wa maisha yao.

 

No comments