KUWA MUAMINIFU, ILA USIMUAMINI MTU

KUNA utofauti kati ya kuwa mwaminifu na kumwamini mtu. Mtu muaminifu ni yule anayefanya yale yampasayo kufanya pasipo udanganyifu au hila yenye nia ofu.
Akipewa kapu lenye maembe mia moja alipeleke
sehemu, atalifikisha kama lilivyo, bila kula embe hata moja njiani kisha huko
aendako, adanganye moja lilioza. Huyu ni mtu muaminifu.
Kumuamini mtu ni kitendo chako cha kuwa na imani
na mtu kwa asilimia mia moja. Yaani, kila jambo lako, hausiti kumshirikisha kwa
kuamini kuwa atakuhifadhi na kukusitiri, iwe jua, iwe mvua!
Nadhani hapo nitakuwa nimeeleweka. Wakati flani
nilikuwa nafanya kazi kwa bosi wangu mmoja hivi, nikisimamia mashine za kamari
ambazo siku hizi zimewekwa baa, ambazo zinaitwa Slots Machine.
Mmoja kati ya wachezaji wakubwa wa kamari zile,
alikuwa ni mzee mmoja hivi ambaye baadaye tulikuja kuwa marafiki sana. Hapo
kabla yangu, kulikuwa na msimamizi mwingine ambaye kuna mambo walikuwa
wanayafanya, kila mmoja akinufaika, sikuwahi kuyaelewa.
Yule mtangulizi wangu alipokuja kuondoka na
kuwekwa mimi, mzee yule akawa hanielewi, lakini akawa anakuja taratibu kutaka
ukaribu. Na kwa kuwa alikuwa ni mteja mzuri, nami nikajisogeza, tukawa
maswahiba!
Siku moja akanialika nyumbani kwake baada ya saa
za kazi. Haikuwa mbali na kazini kwangu, so nikaenda. Nilimkuta na familia
yake, mkewe na watoto wengine ambao tulilingana umri na kumbe tulifahamiana
pia.
Tukiwa peke yetu, yule mzee akanipa mchongo
ambao ulihusu pale kazini kwangu. Kwamba kama ningefanya hivi, kwa pamoja
tungeweza kupata kiasi kikubwa cha pesa. Yaani ilikuwa hivi; hizi mashine
zikichezwa sana, coin zile, yaani hizi sarafu zinazotumbukizwa, hujaa.
Kwa kuwa zamani mashine hizi ziliwekwa katika
vyumba, siyo baa kama hivi sasa, wakati wa kuzitoa hizi sarafu, huja
wafanyakazi maalum kutoka ile ofisi mnafanya nayo kazi, enzi hizo sisi
tukifanya kazi na Las Vegas Casino. Wakija mnafunga milango ili zoezi la kutoa
sarafu lifanyike!
Kwa mfano wakati ule tulikuwa na mashine kama sita
hivi, ambazo wakija kutoa coin zilizojaa, wangeweza kutoa hadi za milioni moja
na ushee.
Kulikuwa na mchezo unachezwa. Wale wafanyakazi wa
casino, walikuwa wanamtumia yule mzee, kutushawishi, kwamba wakati wa kutoa
zile sarafu, kama ni za milioni moja kwa mfano, kule Casino wapeleke labda laki
saba, hizi tatu tugawane. Huu ni mchezo wa kila wiki, just imagine hii ni katikati
mwa 1990!
Mimi nikakataa. Nikasema siwezi kwa sababu kubwa
mbili, kwanza ni mgeni pale kazini, halafu pia siwezi kumuamini yeye, yaani
yule mzee. Akaniambia hiyo sababu ya kwanza nimeielewa, ya pili, huniamini kwa
nini?
Nikamwambia nitajuaje kama hajatumwa na mabosi
wangu kunichunguza? Ajabu, badala ya kukasirika na uhusiano wetu kuanza
kuzorota, ndiyo kwanza ukashamiri na hakuwahi tena kuniambia habari zile ila
aliniambiaga sentensi moja kwamba Uaminifu Unalipa!
Yeah, huo ni mfano unaonihusu. Katika maisha yetu
ya kila siku, haya mambo tunakutana nayo. Uaminifu, wengine wanasema ni mtaji.
Ukijitahidi ukawa muaminifu leo, kesho unaweza kukupatia kazi, maisha, rafiki
au hata jambo ambalo hukulitegemea.
Uaminifu ni ile hali ya kuridhika na hali yako
na kuibana nafsi iache tamaa. Uaminifu si katika fedha tu, hata katika maisha
ya kawaida mitaani. Mtu kakukaribisha nyumbani kwake, unaishi naye kama ndugu,
acha tamaa ya kingono ya kumtamani mwanaye, mkewe au ndugu yeyote pale!
Umepata kibarua, unalipwa kidogo, lakini kuna
vitu ukivichukua, huku mtaani unapata hela zaidi. Achana na hizo tamaa, mwenye
mali anajua kuna nini pale alipokuweka, anapima imani yako tu. Ukikomaa na kazi
yako na usiguse kisichokuhusu, huyu mtu anatafuta mtu wa namna yako, huwezi jua
kuna sehemu bora zaidi anahitaji kukuweka, vitu vingine huwa ni mitego
tunawekewa na sisi tunanasa kirahisi.
Hii ni mifano michache, lakini ninaamini
unafahamu ninapojaribu kwenda, kwamba popote ulipo, jitahidi kuizuia nafsi yako
isitamani kisicho chako, ukibanwa sana, omba!
Lakini pia moja kati ya maeneo tunayokosea sana,
ni kuwaamini watu ovyo ovyo. Mmekutana tu huko kibaruani, mara eti kawa mtu
wako wa karibu, no, no, no, tena big no!
Trust nobody my bra. Achana na huyo mtu
mmekutana kibaruani, usimuamini hata mkeo/mumeo. Hapa usinielewe vibaya, kuna
kuamini na kupenda. Mpende mkeo/mumeo, lakini usimuamini 100%.
You know what? Watu waovu katika maisha yako,
hupitia kwa unayemuamini. Wakishaona wewe na flani ni maswahiba wa kushibana,
hupitia kule. Sasa kama huyo swahiba wako umemuachia mlango wazi, anajua kila
kilichomo ndani mwako, anajua unapoweka silaha, anajua udhaifu wako, anajua
unachokitegemea, kuna nini tena hapo?
Usiruhusu hili jambo litokee. Hata mke/mume wako
kuna mambo hapaswi kujua kwa sababu nani anajua kuwa kesho mnaweza mkawa
maadui? Kuna baadhi ya silaha ni zako peke yako, utazitumia pale mtu wako wa
karibu atakapotaka kuwa tishio, maana hatajua kama unazo.
Ishu siyo kukorofishana na mtu wako wa karibu,
ujumbe hapa ni kwamba usiyaanike maisha yako kwa mtu mwingine ye yote, jitahidi
kadiri unavyoweza, mambo yako ya msingi yabaki kuwa ya kwako. Binadamu, hasa
sisi ngozi nyeusi hatupendani, leo utajianika kwa huyo unayedhani rafiki yako,
kesho mtaa mzima wanajua ulivyo. Unatembea uko uchi, mwenyewe unajiona umevaa
nguo!

Post a Comment