JACQUELINE NTUYABALIWE ANA LAKE JAMBO

JACQUELINE Ntuyabaliwe,
aliyekuwa mke wa pili wa Marehemu Reginald Mengi amesema mumewe hakuwa na
matatizo ya akili kama inavyodaiwa na
kuwataka wanaotoa madai hayo kuacha
uzushi.
Ameeleza hayo
kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Twitter, ikiwa zimepita siku
tatu tangu Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuukataa wosia uliokuwa ukidaiwa
kuandikwa na Mengi ambaye alikuwa mfanyabiashara maarufu nchini ambapo pamoja
na mambo mengine ikieleza kuwa haukidhi matakwa ya kisheria ili kuwa wosia halali.
Katika maelezo yake
aliyoyatoa jana Alhamisi Mei 20, 2021 mlimbwende huyo wa Tanzania mwaka 2000
amesema wanaoibua uzushi huo wanaweza kusema chochote wanachojisikia na
kuchukua mali zote lakini hawezi akakaa kimya na kuacha wamchafue Mengi,
atasimama na kumtetea katika hilo.
“Hii ni ripoti yake
ya hospitali, huu ni kweli kwa wale ambao wanataka kupata uhakika. Mume wangu
hakuwa na matatizo ya kiakili.”
“Mnaweza mkasema
chochote mnachojisikia na kuchukua kila kitu lakini kwa hili nitamtetea hadi
umauti wangu utakaponifika. Daktari Kaushik Ranchod kutoka Afrika Kusini na
daktari Anthony Rudd kutoka Uingereza wanaujua ukweli kuhusu hili,” amesema
Jacqueline aliyeambatanisha picha ya ripoti ya hospitali ya Mengi aliyefariki
dunia Mei 2, 2019.
Uamuzi wa Mahakama
Kuu ulitolewa Jumanne Mei 18, 2021 na Jaji Yose Mlyambina kufuatia shauri la
mirathi lililokuwa limefunguliwa na watu wanne wakiwemo ndugu wa marehemu,
wakiomba kuteuliwa kuwa wasimamizi wa mirathi hiyo.
Jaji Mlyambina
amefikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi lililowekwa na
mmoja wa watoto wakubwa wa marehemu Mengi pamoja na ndugu yake marehemu Mengi,
waliokuwa wakipinga uhalali wa wosia huo ambao pamoja na mambo mengine
uliandikwa kuwa watoto wakubwa wa Marehemu wasipewe chochote katika mali za
Marehemu na kama wataenda Mahakamani kupinga wosia huo wakishinda kesi wapewe
shilingi elfu moja tu (Tsh 1000/=) katika mali za Marehemu Baba yao.
Shauri hilo la
mirathi namba 39 la mwaka 2019 lilifunguliwa na Benson Benjamin Mengi, William
Onesmo Mushi, Zoebu Hassuji na Sylvia Novatus Mushi wakiomba kuteuliwa kuwa
wasimamizi mirathi hiyo kwa mujibu wa wosia huo.
Hata hivyo, mtoto
wa marehemu Mengi, Abdiel Reginald Mengi na ndugu wa Mengi, Benjamin Abraham
Mengi, waliweka pingamizi dhidi ya wosia huo, wakipinga uhalali wake huku
wakiwasilisha jumla ya sababu nne za kuupinga.
Sababu hizo ni
pamoja na kwamba haukwa umepigwa mhuri na saini iliyokuwepo ilikuwa ni tofauti
na saini ya kawaida ya marehemu Mengi na kwamba haukushuhudiwa na ndugu au mke
wa marehemu.
Pia walikuwa
wakidai kuwa marehemu hakuwa na uwezo wa kuandaa wosia kwa kuwa alikuwa na
matatizo ya kiafya tangu mwaka 2016 na kwamba unaondoa katika urithi, watoto
bila kuzingatia mila za Kichaga au kuhusisha ndugu.
Mahakama Kuu baada
ya kusikiliza hoja za pande zote katika hukumu yake iliyosomwa na Jaji Mlyambina
na nakala yake kupatikana kwa matumizi ya umma, alikubaliana na hoja za
pingamizi hilo dhidi ya wosia huo na kuikataa kuwa ni batili.
Jaji Mlyambina
alikubaliana na sababu hizo za pingamizi na pamoja na mambo mengine, amesema
kuwa inawanyima urithi wanaye bila kutoa sababu, na kwamba ziliiingizwa mali za
mke wake mkubwa.
Kwa uamuzi huo,
Jaji Mlyambina hakuwateua waombaji hao kuwa wasimamizi wa mirathi na badala
yake aliwateua Abdiel na Benjamini kuwa wasimamizi wa mirathi na akaelekeza
mali za marehemu zigawiwe warithi wanaostahili kwa utaratibu wa kawaida kama wa
mtu ambaye hakuacha wosia.
Awali mjane wa
marehemu Mengi, Jacquiline alijaribu kuingia katika shauri hilo bila mafanikio
baada ya mahakama hiyo kutupilia mbali maombi yake mara tatu.

Post a Comment