BASHIRU: WAMESHINDWA KUTUGOMBANISHA, WAMELEGEA
MBUNGE wa kuteuliwa na Rais, ambaye kabla alikuwa Katibu Mkuu wa CCM na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Bashiru Ally amesema majaribio yaliyolenga kuwagombanisha Watanzania yameshindwa na kulegea.
“Nchi yetu imepita katika kipindi kigumu cha kihistoria
ambacho hatujawahi kuipitia kutokana na msiba mkubwa uliotukumba, kulikuwepo
majaribio ya kutuchonganisha na wakati mwingine kudhalilisha watu na kutunga
maneno ya uongo ili nchi itikisike, lakini wameshindwa na wamelegea,” amesema
katibu mkuu huyo wa zamani wa CCM.
Dk Bashiru ameeleza hayo bungeni mjini Dodomakatika mjadala
wa bajeti ya Wizara ya Kilimo ikiwa ni mara yake ya kwanza kuzungumza bungeni tangu
alipoteuliwa na Rais Samia Suhulu Hassan Machi 31, 2021.
Bila ya kutaja ni maeneo gani na watu gani waliokuwa
wakiwagombanisha Watanzania na kuwazushia uongo, amemshukuru Mungu kwa kuwa
Rais Samia na makamu wake, Dk Philip Mpango wameonyesha dira na matumaini ya
Tanzania kwa siku za usoni.
Dk Bashiru aliteuliwa kuwa mbunge akiwa amedumu kwa wiki tano
katika wadhifa wa katibu mkuu kiongozi baada ya kuteuliwa na Hayati John
Magufuli Februari 26, 2021.
Nyota ya uteuzi kwa Dk Bashiru ilianzia Mei 2018 alipoteuliwa
kuwa katibu mkuu wa CCM baada ya kufanya vizuri katika kamati ya kuchunguza
mali za chama hicho tawala nchini Tanzania.
Spika Job Ndugai alimuweka kuwa mchangiaji wa mwisho na kumpa
dakika 10 wakati wabunge wengine walikuwa wakipewa dakika tano.
“Mimi ni mteuliwa kati ya nafasi za rais na hadi sasa tupo
wanane, nataka nimuahidi rais kuwa sitamuangusha katika nafasi hii
aliyoniamini,” amesema huku akiendelea kuchangia kuhusu masuala ya kilimo.

Post a Comment