UKINIZINGUA TUTAZINGUANA

 

NI kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan 'Sasha' wakati akitoa nasaha zake baada ya kuwaapisha Makatibu Wakuu wa Wizara na Manaibu wao, Wakuu wa Taasisi za serikali na viongozi wengine kwa ujumla, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Ghafla, umekuwa msemo mkubwa, maarufu na unaotumiwa na wengi kama kibwagizo, huku dalili za awali zikionyesha watu wengi wanamuunga mkono rais huyo wa kwanza mwanamke hapa nchini.

Katika kipindi kifupi tangu akabidhiwe ofisi kufuatia kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, John Pombe Magufuli aliyetangazwa kufariki Machi 17, 2021, Madame Sasha amezungumza mambo mengi yanayotoa ishara ya kurekebisha baadhi ya vitu ambavyo  vilifanyika enzi za mtangulizi wake.

Vitu hivyo ni kama ubabe uliokuwa ukitumika wakati wa ukusanyaji kodi, akiagiza weledi kutumika zaidi, ili kuweka mazingira ya kuwavutia na kuwatengeneza walipa kodi wapya na kuwazuia waliopo kufunga au kuhamisha biashara zao.

Mama Samia pia ametaka haki kutendeka, amekataza dhuluma na kubambikia watu kesi za chuki na visasi. Kumekuwa na kelele kutoka kwa baadhi ya watu wakidai maofisa wa serikali kutumia mamlaka yao kuwapa kesi ambazo hazina ushahidi, kama vile uhujumu uchumi.

Aliwaagiza maofisa wa serikali kuzifuta kesi zote zinazoidhalilisha kwani zinapelekwa mahakamani, lakini zinashindwa. Jambo hili lilipokewa kwa faraja na matumaini.

Ndani ya kipindi kisichozidi mwezi mmoja, Rais Samia Suluhu Hassan, pia amefanya mabadiliko katika taasisi za serikali na kutoa maagizo. Kwanza alimsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania na kuiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kufanya uchunguzi wa upotevu wa mabilioni ya shilingi ndani ya taasisi hiyo.

Wakati wa utawala wa mtangulizi wake, vyombo vingi vya habari, hasa magazeti vilifungiwa na vingine kufutwa kwa sababu mbalimbali. Ameagiza kufunguliwa kwa vyombo hivyo ili kuonyesha uhuru wa kujieleza, lakini akielekeza vyombo hivyo kuelekezwa kanuni.

Magazeti kama MwanaHalisi, Tanzania Daima, Mawio na mengineyo, ambayo yaliandika habari za ubadhilifu wa wanasiasa, wafanyabiashara na wakati mwingine kukosoa utawala, yalifungiwa na mengine kufutwa kabisa kwa sababu mbalimbali.

Licha ya magazeti hayo, lakini pia waandishi wengi wa habari walioandika kuhusu ubadhilifu wa mali za umma, wengi walipatwa na madhira mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kupewa kesi za uhujumu uchumi.

Pia sambamba na hiyo, sheria kadhaa zilitungwa zikilenga kuwadhibiti magazeti na waandishi.

 

 

No comments