WAKANDARASI WATAKIWA KUTEMBELEA ENEO LA MRADI KABLA YA KUJAZA ZABUNI
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Wizara yake kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho amewataka wakandarasi
wote wanaoomba kazi za ujenzi wa miradi ya barabara kuhakikisha wanatembelea eneo
la mradi kabla ya kujaza vitabu vya zabuni ili kuwawezesha kuweka gharama halisi
ya mradi husika.
Dkt. Chamuriho ameyasema hayo jijini
Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayosimamiwa
na Wizara hiyo iliyotengewa fedha kwa mwaka wa fedha 2020/21 na itakayokaguliwa
na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ambapo pamoja na mambo mengine Wizara
imeelezea mafanikio yaliyopatikana kwa mwaka huo wa fedha na mikakati yake ya baadae.
“Kumekuwa na tabia za wakandarasi kutotembelea eneo la mradi na kuona fursa
na changamoto zilizopo kabla ya kujaza vitabu vya zabuni hivyo kupelekea kuweka
gharama isiyo halisi na kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo kuchelewa kwa visingizio
vya ukosefu wa malighafi za ujenzi”, amefafanua Dkt. Chamuriho.
Aidha, amewataka wakandarasi kuacha tabia ya kunakili gharama zilizotumika
katika miradi mingine au zabuni zilizotekelezwa sehemu nyingine kwa kuwa gharama
za ujenzi kwa kila mradi hutofautiana kulingana na maeneo husika.
Katika kuhakikisha fedha zinabaki nchini, Dkt. Chamuriho ameeleza kuwa Wizara
imeendelea kuwashikiza wataalam wa ndani katika ujenzi wa barabara, madaraja na
viwanja vya ndege kwa ajili ya kupata ujuzi ili waweze kusimamia miradi mikubwa
ya ujenzi inayoendelea hapa nchini.
“Tunaendelea kuwajengea uwezo kwa kutumia taasisi zinazowasimamia kwa lengo
la kuwainua wakandarasi wazawa ili waweze kunufaika na miradi inayotekelezwa katika
nchi yetu”, ameongeza Waziri huyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Selemani Kakoso, ameitaka
Wizara hiyo kuendelea kusimamia miundombinu inayojengwa kwani Serikali inatumia
fedha nyingi katika ujenzi wake hivyo wahakikishe inatunzwa na kudumu kwa muda mrefu.
“Hakikisheni mnawachukulia hatua stahiki wananchi wanaokiuka
utaratibu ili kuweza kukomesha tabia ya watu kuharibu miundombinu hiyo ambayo imegharimu
fedha nyingi za Serikali”,amesema Kakoso.
Ameipongeza Wizara kwa uzalishaji wa ajira za moja kwa moja na zisizo za
moja kwa moja zinazotokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama vile ujenzi
wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa awamu zote, miradi ya ujenzi wa barabara, madaraja,
vivuko, majengo ya Serikali na viwanja vya ndege.
Aidha,wajumbe wa kamati wameiomba Wizara kuendelea kutoa elimu kwa umma kupitia
vyombo vya habari, vipeperushi, mikutano na semina kuhusu Sheria ya Barabara
Na. 13 ya mwaka 2007.
“Wananchi wanahitaji kuelimishwa kuhusu hifadhi za barabara na kutofanya
shughuli za kijamii kandokando ya barabara na kutopitisha mifugo sehemu ambazo sio
maalumu kwa mifugo hiyo.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu inatarajia kuanza ziara ya kutembelea
baadhi ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na
hiyo wizara , ambapo kwa ujumla kamati hiyo itatembelea mradi wa reli ya
kisasa (SGR), uboreshwaji wa Bandari, Chuo cha Ujenzi cha Morogoro, mradi wa Magomeni
Kota, Ujenzi wa Daraja jipya la Selander pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara za
Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), jijini Dares Salaam.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Post a Comment