Simba inakuzwa au inastahili?



FCC investigates Simba transformation process - The Citizen

Hakuna ubishi kwamba kwa sasa, Simba inacheza soka safi la kuvutia, mashabiki wake wakiubatiza kuwa ni soka biriyani.

Siyo tu inacheza vizuri, lakini pia timu hiyo ina lundo la wachezaji wenye vipaji. Lakini katikati ya ukweli huo, kuna baadhi ya mashabiki wanahisi wekundu hao wa Msimbazi wanakuzwa.

Kwamba ni timu ya kawaida kabisa, kama zilivyo zingine za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu. Wanaifananisha na Kagera Sugar, Mtibwa, Prisons, Mbeya City, KMC, Biashara, Mwadui, Dodoma Jiji, Polisi Tanzania, JKT Tanzania na Namungo.

Je ni kweli mawazo haya yako sawa?

Lolote linaweza kuwa jibu sahihi kutegemea na nini mwandishi atazungumzia. Kwangu mimi nitajaribu kueleza ni kwa nini ninaamini ninavyoamini.

Kimichezo, Simba iko sawa na timu hizo zote pamoja na Yanga na Azam FC, kwani zote zinacheza ligi moja ambayo hutoa bingwa wa nchi anayewakilisha katika michuano ya kimataifa inayohusisha timu zingine mabingwa barani Afrika.

Lakini kama tutazungumza kuhusu viwango vya soka, siyo sawa kuzifananisha timu hizo na Simba, kwa kuwa kiwango chake, licha ya kucheza ligi moja, lakini ni kikubwa.

Karibu asilimia 95 za mecho zote 19 ambazo Simba imecheza hadi sasa, imeongoza kwa kumiliki mpira (ball possession) licha ya kuwa imefungwa mechi mbili na sare tatu.

Ingawa kuna timu zimeshacheza mechi 23 za Ligi Kuu, nne zaidi yake, Simba ndiyo timu iliyofunga mabao mengi (45) na ndiyo iliyofungwa mabao machache zaidi (8). Maana yake ni nini?

Kwamba Simba ndiyo timu yenye washambuliaji hatari zaidi ya timu zote, ikiwa pia ndiyo timu yenye ukuta mgumu zaidi. Kwa tafsiri nyingine, ndicho kikosi chenye safu bora zaidi ya kiungo, kinachofanya kazi nzuri ya kuunganisha mabeki na washambuliaji.

Huu ni ubingwa wa tatu mfululizo wa nchi, ikiufukuza ubingwa wa nne msimu huu. Yanga, yenye michezo 23 tayari dimbani, inaongoza ligi ikiwa na pointi 50, tano mbele ya Simba, ambayo ina mechi nne mkononi.

Endapo Simba itashinda mechi hizo (Uwezekano huo upo) itafikisha pointi 57, ikimaanisha itawaacha Wananchi kwa pointi saba.

Kuthibitisha ubora wa kikosi hicho chini ya kocha wao Mfaransa Didier Gomez Da Rosa, Simba inaongoza katika kundi lao kwenye ligi ya mabingwa barani Afrika, ambako kabla ya kuanza, iliwekwa nafasi ya nne na ya mwisho kwa ubora.

Imekuwa klabu ya kwanza kutoka Tanzania kupata pointi nne ugenini katika michuano hiyo, ikishinda nyumbani kwa AS Vita kule Kinshasa na baadaye kuitunishia misuli El Merreikh jijini Khartoum, hiyo ikiwa ni pamoja na kuwapiga mabingwa watetezi wa Afrika, Al Ahyl, mchezo uliofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Na katika michezo hiyo yote, kiwango cha Simba kilikuwa juu kuliko timu hizo zote. Wanaonekana wakicheza kwa uelewano mkubwa na kujiamini, bila kujali kama wanacheza nyumbani au ugenini.

Na kwa mara nyingine tena, Simba inakuwa timu ya kwanza kuwapa imani watanzania kuwa itafuzu hatua za makundi msimu huu ikiwa kinara. Wapo wanaoamini pia kuwa timu hii inao uwezo wa kuingia fainali na hata kutwaa taji hilo.

Haya ni mambo ambayo yanaleta utofauti mkubwa kati ya Simba na timu zingine zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara. Licha ya kucheza ligi moja, lakini siyo timu zote hizo zinaweza kuifunga Al Ahyl nyumbani.

Kama kuna mtu anaikuza Simba, anayo sababu ya msingi ya kufanya hivyo na kama yupo anayeishusha, ni kutegemea tu na kwamba anataka kuifananisha na timu zipi, lakini ni kama hizi za ligi kuu, anaweza kuwa ana sababu binafsi zisizo za kimchezo.

 

 


No comments