RAIS SAMIA AAPISHWA, AHUTUBIA, ASIFIWA KILA KONA
JAJI
Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma,
asubuhi hii amemuapisha Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kuchukua nafasi ya Dkt. John Pombe Magufuli aliyetangazwa kufariki
Jumatano jioni.
Katika
hafla hiyo iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan
ambaye anakuwa Rais wa kwanza mwanamke na wa sita wa Tanzania, alikagua gwaride
rasmi lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania kisha akapata nafasi
ya kulihutubia Taifa.
"Nakishukuru chama changu kwa kuwa karibu nami tangu
tulipopata msiba huu mkubwa. Nawashukuru pia viongozi wa vyama vya upinzani kwa
wingi wa salamu za rambirambi na kunipa pole tangu nilipotangaza kuondokewa na
mpendwa wote Rais Dr.John Pombe Magufuli. Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu,
sio wakati wa kutazama yaliyopita. Ni wakati wa kushikamana pamoja kama taifa,
tufutane machozi na tusonge mbele" alisema katika hotuba yake.
Wakati hayo yakifanyika, wadau mbalimbali,
wakiwemo wanamichezo, wasanii na wanasiasa wa ndani na nje ya CCM, wamemmiminia
sifa mwanamke huyo wa kwanza kuwahi kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.
Licha ya kumpongeza na kumtia nguvu, pia
wameelezea imani kubwa waliyonayo juu yake, wakiamini anao uwezo wa kuitendea
haki nafasi hiyo kubwa kabisa ya uongozi wa nchi.

Post a Comment